Je mtandao wa kijamii wa TikTok waweza kuwa fursa kwa biashara?

Written by Shukuru Amos

I am the founder of Tanzlite Digital, Creator, Author of Mbele Ya Muda, and the most followed Tanzanian marketer on LinkedIn.

Posted October 4, 2019

Maisha yanakimbia kwa kasi sana. Miji inazidi kuwa ya kisasa na yenye kupendeza. Umri nao unatutupa mkono vilevile. 

Siku hizi ukilala, ukiamka kuna jambo jipya limeibuka. Mitindo tofauti tofauti ya mavazi, muziki na mengine inakuja na kuondoka kama maji yatiririkayo chini ya daraja la mto uendao kasi. 

Ukija upande wa teknolojia ndio usiseme kabisa. Leo iPhone imetoka mpya kesho Samsung katoa kitu kikali zaidi. Hujakaa sawa Huawei anamtikisa Mmarekani kwa teknolojia ya 5G. Hapa tunaoteseka ni sisi. Hela zenyewe ziko wapi za kuweza kuwa na kila toleo jipya? Wacha tubaki na tecno zetu bwana! 

Turudi kwenye mada yetu;

Tunapozungumzia biashara za karne ya 21, tunagusa moja kwa moja maswala ya digitali, likiwemo suala la mitandao ya kijamii. Mitandao hii imekuwa nguzo muhimu kwa wafanyabiashara kuweza kutangaza bidhaa na huduma zao pamoja na kujenga mahusiano mazuri na wateja wao. 

Ninafahamu unatumia mitandao ya kijamii hasa ile maarufu kama Instagram, Facebook na Twitter. Huenda ukawa umekutana na makala hii kwenye moja ya mitandao hiyo. 

Lakini kuna mtandao mmoja unakuja kwa kasi sana kwa sasa. Unaitwa TikTok. Endelea kusoma kuona ni nini kipya juu ya mtandao huu. 

Takwimu zinasemaje kuhusu mtandao wa TikTok?

Kwa kipindi cha miaka minne tangu kuanzishwa kwake mwaka 2016, TikTok imeweza kuwa na watumiaji zaidi ya milioni 500 duniani kote. Wengi wa watumiaji hawa wakiwa ni vijana. 

ALSO READ:  Jinsi ya Kupata Wateja Mtandaoni Kupitia Matangazo Mguso (PPC Advertising)

Ripoti ya Globalwebindex ya mwaka 2019, inaonyesha asilimia 41 ya watumiaji wa TikTok wana umri kati ya miaka 16 na 24 (Globalwebindex, 2019). Kati ya watumiaji hao, watu zaidi ya milioni 150 hutumia application hiyo kwa siku. 

Aidha, imeripotiwa kuwa application ya TikTok imeongoza kwa kupakuliwa (downloaded) kwenye App Store ya Apple mwaka huu wa 2019. Kuhusu takwimu zaidi, tembelea chapisho la Kiingereza kupitia kiungo hiki

TikTok ina kipi cha tofauti?

TikTok inawapa watumiaji uhuru wa kutengeneza vipande vifupi vya video (visivyozidi sekunde 15) vikinakshiwa na nyimbo na urembo mwingine (filters) wa kuvutia kwa kutumia simu zao za mkononi. Video hizi zimejaa furaha na ucheshi (funny). 

Ukitofautisha na mitandao mingine kama Twitter na Instagram, mitambo (algorithm) ya TikTok inakuonesha vitu unavyovitaka tu. Sio mara unakutana na post ambayo hata hujui imetoka wapi kama inavyotokea huko Twitter na Insta. Pia matumizi ya hashtag yanatamba sana kwenye mitandao huu. 

Wanasema utamu wa ngoma ingia mwenyewe ucheze. Pakua application ya TikTok uonje utamu wake.

Ukiitizama vizuri application ya TikTok utaona ina muonekano sawasawa na application inayoitwa Musical.ly. Hii ni kwa sababu TikTok ambayo ni kampuni ya Kichina, iliinunua application ya Musical.ly ili kuweza kuwafikia watu wengi hasa vijana wa kimarekani. 

ALSO READ:  Fahamu Fursa Nne Zinazopatikana Kidigitali

Swali; Je TikTok inaweza kuwa fursa mpya kwa wafanyabiashara? 

Kwasasa TikTok haina mfumo wowote unaowezesha kuweka matangazo ya kulipia (sponsored ads) kama tunayoyaona huko kwenye mitandao mingine. 

Lakini kama tunavyofahamu, hakuna kitu cha bure. Nionavyo mimi, jukwaa hili halitakuwa la bure kwa mda mrefu.

Kwa kuwa mtandao huu unapendwa na vijana wengi ambao ndio wenye nguvu ya ushawishi katika masoko, ninaona kuna kila dalili ya makampuni makubwa (brands) kuishawishi ikubali TikTok ikubali matangazo. 

Baadhi ya takwimu zinatabiri mtandao wa TikTok utakuja kuteka na kuizidi mitandao kama vile Instagram na Snapchat.

Changamoto kubwa ya mitandao ya kijamii ni tabia yake ya kubadilika kila mara, kwa kuja na mifumo mipya au kupotea kabisa kama mtandao uliokuwa ukimilikiwa na kampuni ya Google, uliofahamika kwa jina la Google+

Lakini pia ni lazima tukubaliane na ukweli kwamba hatuwezi kukwepa social media. Mitandao hii imewapa nguvu watumiaji kuwa na uhuru wa kuchagua ni namna gani wanataka kupokea taarifa. Hivyo kama mfanyabiashara unaetafuta kukuza jina la biashara yako na kufikia wateja wengi zaidi, huna budi kuwekeza kwenye moja ya mitandao hii. 

Palipo na wengi pana fursa nyingi. Wewe kama mfanyabiashara, unajiona uko tayari kuwafata wateja wako walioko TikTok? Au utawasubiri wakirudi Insta na Fb? 

0 Comments

Submit a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

You May Also Like

Products From Tanzlite