Fahamu Fursa Nne Zinazopatikana Kidigitali
Mara nyingi umekuwa ukisikia watu wanaongelea kuhusu fursa unazoweza kufanya kupitia majukwaa ya kidigitali lakini bado hujajua hizo fursa ni zipi, na unawezaje kuzipata? Kwenye makala hii nitakuelezea kwa ukaribu hizo fursa, namna ya kuzipata na jinsi ya kuzitumia ili kujiingizia kipato.
Majukwaa ya kidigitali yamekufungulia dunia kuwa unachotaka, fursa zote unazo kiganjani mwako. Unaweza kufanya biashara yako binafsi kupitia hii hii mitandao na kujipatia kipato au kufanya kazi na mtu yeyote kutoka sehemu mbalimbali bila kuonana uso kwa uso.
Kitu chochote unachoweza kufanya kidigitali na kikakuletea faida hiyo ni fursa.
Mfano, Natoa huduma za kupamba kumbi za sherehe, nitaanza kushare picha zikinionyesha napamba kumbi mbalimbali kwa ajili ya sherehe tofauti kama harusi, mikutano, sendoff au kitchen party ili atakayeona na kuvutiwa anitafute tufanye kazi.
Hivyo ndio jinsi fursa za kidijitali zilivyo kuuza ujuzi au bidhaa zako mtandaoni kwa watu wengi kwa mara moja. Kuna Aina nyingi za Fursa mtandaoni ni wewe tu kuchagua ipi itakufaa
1. Kuuza Huduma zako(Services)
Hii inaweza kuwa huduma unayoitoa wewe mwenyewe binafsi au kama kampuni. Mfano kufundisha au kusherehesha. Dukahuru anapatikana Instagram akifundisha watu wengine jinsi ya kuuza bidhaa mtandaoni na huduma nyingine nyingi.
Kama wewe unaweza kufanya hivyo basi hiyo ni fursa ikimbilie mapema.
Huduma ya kikampuni ni kama ile anayofanya Haika Lawere anakodisha kumbi zake kwaajili ya sherehe, vikao au makongamano. Pale instagram huwa anapost picha za kumbi, bei na mawasiliano kwa atakayehitaji.
Wewe kijana au wewe ndugu yangu uliye kwenye kampuni na una matazamio ya kupata chochote kutokana na hilo kampuni unalofanyia kazi, tumia muda huo kuji-promote kwa kutumia status ya kampuni ili hata siku umetoka, utoke na jina.
Kwa yule mwenye uwezo wa kufanya kama Haika basi fanya, hiyo pia ni fursa itakayofanya usihangaike kutafuta fursa zingine.
2. Kuuza bidhaa zako binafsi (Products)
Mfano; unamiliki duka la kuuza mafuta ya nywele, una simu janja, jiunge mtandao wa Instagram, fungua kurasa yako na anza kupost mafuta yako unayouza, kumbuka jinsi utakavyojinadi katika bidhaa yako ndivyo utakavyoweza kupata wateja.
Hapa nazungumzia jinsi ya kupost(maudhui). Watu mbalimbali wataona bidhaa yako na watakutafuta ili hali uliweka mawasiliano kwenye kurasa yako.
Je, ushawahi kununua kitu mtandaoni? Kama jibu ni ndiyo basi hata wewe unaweza kuuza kitu chochote mtandaoni. Unahitaji tu kujua wateja wako wanapatikana mtandao upi, jifunze jinsi ya kutumia mtandao husika vizuri na upeleke biashara yako huko.
3. Kuuza bidhaa za watu wengine (Affiliate Marketing)
Kama hauna mtaji wa kuanzishia biashara yako na hauna biashara yoyote unayoifanya. Tafuta kampuni au biashara ya mtu ambaye utakuwa unamsaidia kutafuta wateja mtandaoni au kufanya biashara yake ijulikane kwa watu wengi.
Mtu anayefanya kazi ya affiliate marketing hulipwa kutokana na mauzo yatokanayo na juhudi zake za kuleta wateja. Hii unaweza kuifanya kwenye blog, tovuti yako binafsi au kwenye mitandao ya kijamii.
Pia kuna makampuni yana bidhaa zao na yanatafuta watu wa kuwasaidia kuuza au kuwafikia wateja na kwa kila mteja utakayemleta utapewa Kamisheni.
Kamisheni ndo itakua faida yake kutokana na makubaliano mtakayoweka.
4. Kushawishi watu kununua bidhaa Fulani (Influencing)
Hii inatumiwa sana na makampuni mbalimbali makubwa na madogo. Kutafuta watu wenye ushawishi mtandaoni kuweza kushawishi watu watumie huduma au bidhaa zao. Na utalipwa kwa makubaliano mtakayoweka. Mfano Lilian Lema anafanya hii kazi Instagram na kulipwa.
Utahitaji kuwa na page yako ambayo umeijenga mwenyewe na kupata wafuasi ambao utaweza kuwashawishi. Sio lazima uanze ushawishi kwa kulipwa unaweza fanya bure na badae ukaanza kuchaji watu wakitaka huduma hiyo kwako.
Hili ndo somo langu la leo kuhusu fursa za kidigitali, haimaanishi ndio mwisho wa fursa, Hapana. Kutokana na hizo nne unaweza pata fursa nyingine zaidi. Muhimu ni kujiamini unaweza na kuanza kufanya.