Usalama Mtandaoni ni nini? Umuhimu na Jinsi Ya Kuwa Salama.
Inawezekana wewe ni mmiliki wa simu janja, kompyuta au kifaa kingine kama hivyo. Kama hivyo lazima unatumia mtandao kwa shughuli zako mbali mbali iwe kupata taarifa, kuwasiliana, kufanya malipo au kutoa au kupata huduma mbalimbali.
Lakini je unafahamu kuhusu usalama wako wakati wa utumiaji wa mtandao? Wengi hatufuatilii kuhusu usalama wa mtandaoni hasa kwenye kutoa taarifa binafsi ambazo zinaweza kudukuliwa na kumpa mtu nafasi ya kufanya uhalifu mtandaoni.
Ushasikia stori za watu au makampuni kuibiwa pesa, akaunti za kijamii au taarifa flani nyeti kwa ajili ya kufanyia utapeli mtandaoni?Hii yote inatokana na ukosefu wa uelewa kuhusu usalama mtandaoni.
Kama wewe ni mtumiaji mzuri wa mtandao basi Makala hii ni maalum kwa ajili yako kupata uelewa kuhusu usalama mtandaoni. Ni nini na jinsi gani unaweza kujiweka salama mtandaoni.
Usalama mtandaoni ni nini?
Ni utumiaji wa mtandao unao fuata kanuni, sheria na tahadhari ili kujihakikishia usalama katika matumizi yako ya mtandao. Hatua hizi husaidia katika ulinzi wa taarifa zako binafsi zidi ya hatari zinazoletwa na matumizi teknolojia na intaneti. Hatari hizo hufaamika kama uhalifu wa mtandaoni ‘Cybercrime’.
Kuna umuhimu gani wa kuwa salama mtandaoni?
Kwa sababu vifaa vya kidijitali unavyotumia vinabeba taarifa mbalimbali binafsi ambapo mtu mwingine akizipata anaweza kuzitumia kwa uhalifu. Taarifa hizo zinaweza kuwa nywila, hifadhidata ‘database’ za matukio mbalimbali au ripoti muhimu.
Taarifa hizi zinaweza kuwa za mtu binafsi, taasisi za umma, mashirika binafsi au Serikali. Endapo kifaa chako unachotumia kitaibiwa au kupotea bila kuwa na ulinzi wowote, basi ni rahisi sana mtu kutumia nafasi hiyo kuchukua taarifa muhimu zilizohifadhiwa na kutumia nje ya kusudi lililopangwa.
Ni kwa jinsi gani mtu anaweza kujiweka salama mtandaoni?
- Tambua kundi la kifaa unachotumia kuingia mtandaoni.
i. Kundi la vifaa binafsi kama vile simu janja, kompyuta binafsi au saa janja.
Vifaa hivi hubeba taarifa nyingi, programu na data mbalimbali kukuhusu. Hivyo njia ya kujiweka salama ni kufunga kifaa chako kwa njia za kiusalama zinazojulikana mfano pini namba, nywila, kitambua uso au alama ya kidole.
Kutompa mtu nywila yako uliyoweka kwenye kifaa chako. Usipende kuruhusu mtu yoyote kufungua kifaa chako na kuperuzi kifaa chako kwenye program mbalimbali zilizopo kwenye kifaa chako. Kuhakikisha program zako zimesasishwa kwa toleo la sasa.
ii. Kundi la vifaa vya umma/ ushirika
Hivi vinaweza kua vya ofisini, nyumbani au kwenye sehemu za kutolea huduma ya intaneti kama intaneti café. Mara nyingi huwa ni komputya za mezani na hujumuisha watumiaji Zaidi ya mmoja. Hivyo umakini unatakiwa zaidi.
Kuwa salama kwenye vifaa hivi ni kuhakikisha unatoka kwenye wasifu wako kila baada ya kumaliza matumizi yako. Kutoruhusu eneo la kujaza nywila liwe automatiki kwani litafanya yoyote yule aweze kuingia kwenye akaunti yako bila kizuizi. Pia unaweza kufuta historia yako baada ya kumaliza kutumia.
2. Tambua aina ya mtandao umeunganishwa nayo (Binafsi au Pamoja)
Kuna wanaotumia mtandao wa Binafsi na kuna wanaotumia mtandao usio na waya ‘wi-fi’. Mtandao usiokua na waya huruhusu watumiaji zaidi ya mmoja kuunganishwa. Hivyo kuhitaji umakini Zaidi na kujilinda kuepusha kudukuliwa.
Mtandao usio na waya ‘Wi-Fi’ Ukitumia na kujiunganisha ni vyema ukabadilisha jina la kifaa chako na nywila ili watu wasiweze kujiunga bila ruhusa yako.
3. Uhakiki wa Programu unazotumia
a. Programu za simu – Programu nyingi huhitaji kujaza taarifa zako ili uweze kutumia. Pia programu nyingine huunganishwa na program nyingine kupata taarifa zako mbalimbali hivyo kuwa salama unahitaji kupakua program kutoka kwa mtengenezaji anayetambulika.
b. Linki za kuingia tovuti mbalimbali- muhimu ni kuhakiki jina sahihi la tovuti ‘domain name’. Kwani wahalifu wengi hubadili jina halisi na kuweka tofauti ndogo ambayo sio rahisi kugundulika.
Hakikisha unafungua linki yenye https mwishoni kuashiria usalama wako. Na sio yenye http maana taarifa zako zitakua wazi.
Unaweza kutumia kifaa chako katika hali ya faragha, hii huzuia kuweka historia ya matumizi. Lakini pia epuka kufanya malipo mbalimbali hasa ya kifedha kwa kutumia kifaa cha umma, kwani ni rahisi kudukuliwa.
Usalama mtandaoni hasa kwa watumiaji wa mitandao kama sehemu yao ya kazi ni muhimu zaidi. Inawezekana ulikua hujui umuhimu wake.
Bado hujachelewa, Anza sasa! Makala hii iwe muongozo wa usalama wa matumizi yako mbalimbali ya mtandao ili kuepukana na uhalifu.