Ukweli Kuhusu Kupata Wateja Mtandaoni (Darasa Muhimu)

Ukweli Kuhusu Kupata Wateja Mtandaoni (Darasa Muhimu)

Watu wengi wanalalamika biashara zao hazipati wateja mtandaoni pamoja na kwamba wanapost bidhaa zao Instagram, WhatsApp na kwenye majukwaa mengine ya digitali.

Wengine huanza kufikiri pengine kufungua website itasaidia kupata wateja kuliko kuwa na Instagram au WhatsApp pekee.

Wengine hudhani kununua akaunti yenye followers wengi basi itasaidia kupata wateja. Wanatafuta akaunti inayouzwa, yenye followers 10K au zaidi, wananunua. Lakini bado hawapati wateja. Na hata kile wanachokipost hakipati likes wala comments pamoja na kuwa na followers wote hao.

Hata matangazo ya kulipia (sponsored ads) hayawasaidii. Wanajikuta wanapoteza pesa tu.

Wengine wanawalipa “wataalamu” wa social media wanaojitangaza wanakuza akaunti na kuongeza followers. Followers kweli wanapata, lakini kuuza bado inabaki changamoto!

Hayo yote niliyoyataja hapo juu ni baadhi ya malalamiko tunayopata kila wiki kutoka kwa wajasiriamali wanaouza bidhaa mtandaoni. 

Malalamiko haya pamoja na maswali mengine tunayapata kupitia kampuni yetu,Tanzlite Digital, inayosaidia wafanyabiashara kukuza biashara zao na kujipatia wateja kupitia majukwaa ya digitali.

Malalamiko ni mengi. Nitatumia  makala hii kueleza ukweli kuhusu kupata wateja mtandaoni.

Nini Kinafanya  Watu Wanunue Bidhaa yako Mtandaoni?

Zipo sababu kuu tatu zitakazokufanya uuze bidhaa mtandaoni: 

  1. Soko na Bidhaa yenyewe.
  2. Jina lako mtandaoni (Watu wanakufahamu?)
  3. Uwezo wako kushawishi kupitia Maudhui.

Ubora na Soko la Bidhaa Yako

Hapa naomba tuelewane. Kama kitu unachokiuza ni kile ambacho watu wanaweza kukipata kwa urahisi mtaani kwao —basi hutopata wateja mtandaoni. 

Kwanini wanunue kwako wakati bidhaa hiyo hiyo inapatikana kwa mangi au na maduka mengine ya karibu?

Jiulize; unaweza kuuza soda mtandaoni? Au wembe au majani ya chai? 

Kama kila mtu anauza kile unachotaka kukiuza mtandaoni basi inabidi uwe na OFA nzuri, au kuwe na ubunifu na namna ya uwasilishaji bidhaa yako kwa watu ili kujitofautisha na wengine. Vilevile ujenge mahusiano mazuri na wateja wako ili waendelee kurudi na kuwaambia wengine.

Lakini kwa bidhaa kama vile karanga, mchele, vitenge, na baadhi ya nguo  —hizi zinapatikana kila mahali. Usishangae kuona hupati wateja mtandaoni. 

Watu hawatafuti mtandaoni vitu ambavyo vinapatikana kila kona mtaani kwao. 

Ili kupata wateja mtandaoni, bidhaa yako inatakiwa kuwa na upekee, ubora na soko lake liwe halijachuja (saturated) kwa kuwepo wa utitiri wa bidhaa hiyo kila mahali. Tofauti na hapo, ni bora ufungue duka mahali penye mzunguko mkubwa wa watu (foot traffic). Kama vile Kariakoo.

Mitandao inasaidia kufikisha bidhaa yako kwa watu wengi. Lakini kuuza inategemea na bidhaa yenyewe.

Jina Lako Mtandaoni (Brand Authority)

Kule Instagram wapo watu wanauza bidhaa za aina mbalimbali kama vile nguo, viatu, na electronics. Lakini yapo majina machache maarufu kama vile (kwa Tanzania) Vunja Bei, Frank Knows, David Sportwear, na kadhalika.

Hao na wengine wengi wenye waliojitengenezea jina mtandaoni wanapata wateja na kuuza bidhaa zao.

Unajua kwanini wanauza? Ni kwa sababu watu hupenda kununua kitu kutoka kwa mtu wanayemfahamu, au wamewahi kumsikia, au watu wengine wanamuongelea.

Je wewe umetengeneza jina? Hakuna mtu yuko tayari kukutumia pesa ikiwa hakufahamu, hajawahi kukusikia, wala haoni watu wengine wakikuongelea. Hapa watu kukuongelea maana yake angalau kuwe na comments kwenye post zako mtandaoni.

Naomba nitoe mfano. Kuna watu wanauza bidhaa za makampuni ya network marketing au MLM kama vile BF Suma na Forever Living.

Hawa watu wanashida kubwa. Kwanza kabisa wamepigwa pesa yao ambayo hawataweza kuirejesha kuuza bidhaa hizo. Pili wewe siyo daktari, siyo mtaalamu wa lishe, huna pharmacy, na huna zahanati. Isitoshe huna hata mtu mmoja uliyemponya kwa dawa zako. Dawa yenyewe unasema inatibu “magonjwa mbalimbali”. Kwa kifupi hauna authority ya kumshawishi mtu anunue bidhaa kutoka kwako.

Tatizo siyo bidhaa, tatizo ni nani anauza hiyo bidhaa.

Narudia tena; watu hawanunui bidhaa bali wananunua jina la mtu linalohusiana na bidhaa hiyo. Daktari akikuandikia dawa, unaenda kuinunua na kumeza si kwa sababu unaijua hiyo dawa (inaweza isiwe bora) bali kwa sababu unamwamini daktari.

Nikupe mfano mwingine, hivi majuzi tajiri Elon Musk alitangaza bidhaa mpya ya pefume. Ndani ya masaa machache aliweza kuuza chupa 10,000 kwa bei ya dola za kimarekani 100 kila chupa. Jamaa alitengeneza dola milioni moja ndani ya masaa tu.

Hiyo ndiyo nguvu ya kuwa na jina. Tengeneza jina kwanza halafu kuuza mtandaoni itakuwa rahisi. 

Kutengeneza jina mtandaoni si kuwa maarufu (fame, celebrity). Ni kujenga taswira yenye kuaminika miongoni mwa watu unaowalenga. 

Kumbuka, Kuwa na Jina Mtandaoni Siyo Umaarufu. 

Hapo awali nimesema ili uuze mtandaoni lazima uwe na jina. Hapa simaanishi umaarufu (fame, celebrity). Hapana. Jambo la msingi ni kuhakikisha unatengeneza jina miongoni mwa watu unaowalenga kununua bidhaa yako. Si lazima Watanzania wote wakujue. 

Kama watu 1000 wamekufollow baada ya kuona unachouza basi hilo ndilo jeshi lako. Kama wamekufollow kwa hiari maana yake wamevutiwa na unachokifanya. Endelea kuwapa maudhui bora (waelimishe, wachekeshe, wape mbinu za kutumia bidhaa yako n.k). Hao watu 1000 wanaweza kusambaza habari zako kwa wengine na hivyo ndivyo utakua na kujipatia jina. 

Lengo ni kujiweka katika mazingira mazuri ya kuvutia wateja. Hakikisha profile inavutia, haina makosa au picha zisizo na ubora.

Hapa pia naomba nikazie jambo; kununua followers ni kupoteza pesa zako. Epuka mtu anayekwambia atakupatia followers. 

Uwezo wa Kushawishi Wateja 

Unaweza kuwa na bidhaa nzuri lakini ukashindwa kushawishi wanunuzi. Unaweza kuwa na dawa inayotibu kansa lakini watu wasiamini kwa sababu huna ushawishi. 

Hii ni changamoto ya kushindwa kufahamu saikolojia ya mteja unayemlenga pamoja na kushindwa kuandaa maudhui (content) yenye mvuto na yenye kushawishi. 

Jiulize; zile picha, video na maandishi unayopost mtandaoni yana nguvu ya kushawishi? Yana mvuto? Picha ni kali au ni low quality?

Yote hayo yanachangia kama watu watavutiwa na kukuamini au hawatavutiwa na kukutilia mashaka.

Kwa mfano tuseme unauza pazia. Badala ya kusema; OFA! Jipatie Mapazia Mazuri kwa Bei Nafuu. Tunapatikana Kariakoo

Unaweza kusema; Pendezesha Nyumba Yako kwa Pazia Nzuri Ili Wageni Wakija Waone Kweli Wapo Ndani Ya Nyumba

Wanawake hawanunui pazia bali wananunua UFAHARI wa kupendezesha nyumba. Wakienda kununua pazia swali wanalojiuliza kichwani ni “Pazia gani litapendeza ndani ya nyumba yangu?”. 

Jaribu kucheza na saikolojia ya mteja unapoandaa maudhui ya kupost Instagram au popote unapopatia wateja. Onyesha Matokeo; nini mteja atapata akinunua bidhaa yako? Je atapata mwonekano mzuri? Je chumba chake kitapendeza? 

Katika kuandaa maudhui, onyesha matokeo ya bidhaa. Usionyeshe bidhaa.

Badala ya kupiga picha mabaro ya vitenge dukani kwako, piga picha ya mwanamke aliyevaa kitenge na kupendekeza. 

Badala ya kupiga picha mapazia uliyotundika dukani mwako, piga picha pazia zilizotundikwa ndani ya nyumba. Watu hujaribu kutengeza picha kichwani ya namna gani nguo itaonekana wakiivaa, au pazia litaonekanaje likiwa ndani ya nyumba. Usionyeshe tu bidhaa, onyesha matokeo. 

Ukiwafahamu wateja wako vizuri, na bidhaa yako ikawa iko vizuri, basi hata yale matangazo ya kulipia yatazaa matunda. Vinginevyo utakuwa unachoma pesa.

Hitimisho: Ukweli Kuhusu Kupata Wateja Mtandaoni 

Mitandao ni njia tu ya wewe kufikisha bidhaa yako kwa walengwa. Kuhusu kuuza au kutokuuza inatokana na sababu nyingi ikiwemo bidhaa yenyewe, soko, pamoja na uwezo wako wa kushawishi. 

Kwa ujumla mitandao imerahisisha sana jinsi ya kufikia wanunuzi wa bidhaa za watu. Bila mitandao kama WhatsApp, Instagram, YouTube, Tovuti na mingineyo, watu walio mbali wasingeweza kuona bodhaa yako na kuwasiliana nawewe. 

Kila mtu anaweza kuuza chochote mtandaoni mathalani kitu hicho kina soko na muuzaji anaweza ku-supply hiyo bidhaa.

____________

Asante kwa kusoma makala hii. Naitwa Shukuru Amos, ni mwandishi na mtaalamu wa masoko ya digitali (Digital Marketing). Wasiliana nami kwa WhatsApp hapa

Share makala hii kwa mfanyabiashara mwingine.