Digital Marketing ni nini? Haya hapa mambo muhimu ya kufahamu

Digital Marketing ni nini? Haya hapa mambo muhimu ya kufahamu

Teknolojia imeleta mambo mengi. Mojawapo ni kuibuka kwa kazi ambazo hazikuwepo kabla. Vilevile imeweza kubadili namna ya utendaji kazi wa kazi nyingi tulizozizoea na kuzifanya ziwe tofauti kabisa. Teknolojia imeathiri kila kitu. 

Moja kati ya taaluma mpya zilizoweza kuibuka kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia ni taaluma ya kutafuta masoko na kuuza bidhaa au huduma kwa njia ya kidigitali (Digital Marketing). Taaluma hii kwa hapa nchini Tanzania bado ni ngeni na wengi hawaifahamu. Hata vyuo vyetu bado havijaanza kufundisha somo hili ipasavyo. Lakini sio jambo la kushangaa kwani ni jambo la kawaida kwa vyuo vyetu kuachwa nyuma na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.

Digital Marketing ni nini? 

Mara nyingi ninapojitambulisha kwamba ninafanya digital marketing, wengi huniuliza maana ya digital marketing. 

Katika makala hii utaweza kufahamu maana ya Digital Marketing pamoja na kufahamu sehemu unayoweza kujifunza elimu hii bure kabisa na kupatiwa cheti kinachotambulika duniani. Kama wewe ni mfanyabiashara unayetamani kuingia kwenye ulimwengu wa kutafuta masoko kidigitali au unataka kujifunza Digital Marketing kama taaluma basi makala hii inakuhusu. Twende sambamba. 

Kwa tafsiri ya kawaida, Digital Marketing inaweza kutafsiriwa kama;

Utafutaji masoko, kuuza pamoja na kutangaza bidhaa au huduma kwa kutumia majukwaa ya kidigitali (online platforms) kama vile mitandao ya kijamii na tovuti. 

– Tanzlite

Angalia maana kutoka kwenye mtandao hapa chini;

The use of numerous digital tactics and channels to connect with customers where they spend much of their time online

– HubSpot

The marketing of products or services using digital technologies, mainly on the internet, but also including mobile phones, display advertising, and any other digital medium

Wikipedia

Digita Marketing kwa majina mengine huitwa Internet Marketing, e-commerce au Online Marketing.

Kwanini digital marketing ni muhimu? 

Sababu zinaeleweka. Siku hizi kila mtu yuko online. Kila mtu yuko kwenye mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, Instagram na mingineyo. Mitandao imejaa watu. Wakiwemo wateja wa bidhaa yako. 

Hii ina maana gani kwa wafanyabiashara? 

Wafanyabiashara na wajasiriamali wanatakiwa kujiongeza. Siku hizi mambo ni digitali, hivyo biashara nazo hazina budi kuendeshwa kidigitali. Hauwezi ukaweka mabango barabarani au kubandika kwenye magari wakati watu wanatumia muda mwingi kutazama kwenye simu janja zao. 

Hata redio na televisheni zimekuwa hazitumiwi sana na watu. Siku hizi ni mwendo wa YouTube na muziki wa kudownload. Kila kitu kiganjani. 

Kama mfanyabiashara unaekwenda na wakati, ni lazima kuingia kwenye ulimwengu wa uuzaji na utafutaji masoko kidigitali. Wateja wako wapo Instagram na Facebook kwanini wewe usiwepo? 

Vipengele vinavyo husisha Digital Marketing

Ukisikia digital marketing, mara nyingi Inahusisha vipengele vifuatavyo;

Kutafuta masoko kupitia mitandao ya kijamii (Social Media Marketing) 

Hili ndio swala ambalo watu wengi humaanisha wakiongelea Digital Marketing. Makampuni mengi yamefungua akaunti za mitandao ya kijamii kwa lengo la kujiweka karibu na wateja wao pamoja na kupata wateja wapya, kujenga mahusiano mazuri na wateja wao pamoja na kuzungumza nao wanapokuwa na maswali. 

Kupitia mitandao ya kijamii, kampuni hutengeneza maudhui kwa mfumo wa picha, video au maandishi ili kuwafahamisha wateja kuhusu huduma za kampuni, kutoa ofa na promosheni mbalimbali kwa wafuatiliaji wake (followers) Fahamu zaidi kuhusu kazi ya social media na majukumu yake hapa. 

Uuzaji kupitia barua pepe (Email marketing) 

Umeshawahi kuambiwa Subscribe to our newsletter? Basi hicho ndio kitu tunaongelea hapa kwa haraka haraka. Barua pepe ni mtandao mkongwe ambao umekuwepo kwa miaka mingi sasa. Wafanyabishara huomba kukusanya barua pepe za watembeleaji wa tovuti zao ili baadaye waweze kuwashirikisha juu ya fursa na ofa mbalimbali za kampuni husika. 

Kwa kuwa watu wengi wanatumia simu za mkononi, barua pepe hazina budi kuandaliwa katika muonekano unaofaa kwenye simu (mobile friendly). Bila kufanya hivyo ni bora usitumie njiaa hii kwani email zako hazitasomwa na utawafanya wateja kujiondoa (unsubscribe) kwenye orodha ya mawasiliano yako. 

Kujitangaza kupitia Tovuti (Website) 

Tovuti ndio njia kuu ya kupeleka biashara yako online. Kama ulivyofungua duka la nguo pale Kariakoo, basi unaweza ukalihamisha duka hilo hilo ukalipeleka mtandaoni na wateja wanaweza kukutembelea, kuchagua nguo na kufanya manunuzi bila kufika dukani kwako Kariakoo. Maajabu sio? Fikiria tovuti kubwa kama vile alibaba au eBay. Au hata tovuti za ahapa nyumbani kama vile Kupatana. Jaribu kuwa na tovuti yako ujionee faida zake. Hakikisha website yako ni nyepesi kufunguka, na inapendeza kwenye simu za mkononi. 

Matokeo ya haraka (Search Engine Optimization) 

Kuweka biashara yako mtandaoni si swala la kufungua tovuti tu. Bali tovuti yenye ubora unaotambuliwa na injini za utafutaji (Search Engines). Hii inajumuisha mambo kama maudhui (content) unayoweka kwenye tovuti na ubora uliotumika kujenga tovuti yako (programming). Tovuti iliyojengwa vibaya haiwezi kuoneshwa kwenye matokeo ya utafutaji (Search Results) hivyo kukufanya usiweze kujulikana na kupelekea kukosa wateja.

Fanya utafiti mdogo kuangalia kama tovuti yako inatambuliwa (indexed) na injini ya utafutaji ya Google kwa kuingiza maneno yafuatayo kwenye sanduku la kutafutia (Search bar)  site:yourdomain

Mfano; site:tanzlite.com

Hakikisha matokeo yatakapoletwa na Google yanaonyesha kurasa (pages) zote zilizopo kwenye tovuti yako. Usipoona kitu ujue una kazi ya kufanya. 

Matangazo ya Kulipia (Sponsored Ads)


Kama umeshawahi kukutana na post ya page ambayo huja-follow imeandikwa “Sponsored”, basi hayo ndiyo matangazo ya kulipia. Ni aina ya digital marketing ambapo unatumia pesa kufikisha tangazo lako kwa watu wengi zaidi. Hii ni inasadia kwa mwenye biashara ambaye ndiyo anaanza kuweza kufikia wateja kwa muda mfupi sana.

Unaweza kutumia matangazo ya Facebook, matangazo ya Instagram, Google n.k. Habari njema ni kwamba matangazo haya hayana gharama sana; mfano Facebook na Instagram watakudai dola moja tu kwa siku kama kiwango cha chini cha matumizi.

Matangazo mguso (Paid Per Click Ads) 

Yanaitwa matangazo mguso kwa sababu malipo hufanyika mara tu mtu anapo bofya tangazo lako. Hii ni aina ya kutangaza bidhaa au huduma kwa kununua maneno maalum (keywords) yanayohusu bidhaa yako ambapo mtu akitafuta kwa kutumia maneno hayo, biashara yako inaweza kuoneka juu kwenye matokeo ya utafutaji (search results) 

Graphic design

Ukiingia WhatsApp au kwenye mitandao mingine ya kijamii, utakutana na picha zilizonakshiwa kwa maneno na rangi nzuri. Hii kitaalamu Graphic design (sijui kwa Kiswahili tunaitaje). Basi kila mwenye brand au mwenye event yake anataka kuporomote kwa nakshi zenye kuvutia macho ya watu na kuwashawishi kuisambaza (share) kwa wenzao. 

Kutangaza biashara kwa njia ya video (video marketing) 

Ukiondoa Google, ni search engine gani nyingine ya pili kwa ukubwa? Je ni Bing? Au Yahoo? Jibu ni YouTube. Watu wanaangalia video kwa wingi sana siku hizi . Kwa mfanyabiashara mjanja hii ni fursa kubwa. Unaweza kutumia video kuonyesha ujuzi wako katika huduma unayofanya au kuwaonyesha watu kuhusu mambo yanayojiri ofisini kwako. Pia kutangaza biashara yako YouTube si lazima uwe na video clip, —nitalifafanua hili kwa undani zaidi katika makala zijazo. 

Kutangaza biashara kupitia watu wenye ushawishi mtandaoni (Influencers) 

Watu maarufu mtandaoni wana nguvu ya kushawishi na kuweza kubadili mtazamo wa watu juu ya jambo fulani. Hivyo makampuni na brand mbalimbali zinatumia watu kama hawa kutangaza biashara zao na kufikia watu wengi. Hapa Tanzania kuna watu kama Idris Sultani ambaye ni balozi wa kampuni ya Uber. 

Kukua kwa influencer marketing kumekuja kwa sababu kuu moja; mitandao ya kijamii ni watu, na watu wanapenda kushiriki (interact) na watu wenzao kuliko kampuni. Hivyo makampuni yanajitahidi kuwa karibu na watu kwa kuwatumia watu maarufu kukuza biashara zao. 

Wapi unaweza kujifunza elimu ya Digital Marketing 

Elimu ya Digital Marketing ni moja kati ya elimu ambayo mtu hauhitaji kuwa na degree ya miaka mitatu chuoni. Lakini faida zake ni kubwa hasa katika kipindi hiki ambacho wahitimu wanatoka vyuo wasijue nini cha kufanya mtaani. Nikushauri leo, anza kujifunza Digital Marketing. Hapa chini nimeorodheasha sehemu tatu ambazo unaweza kusoma online course za digital marketing na mambo mengine mengi.

  1. LinkedIn Learning 
  2. Google Digital Skills for Africa 
  3. HubSpot Academy 
  4. The Future Learning

Ingia mtandaoni leo, chagua kozi na uanze kusoma. Ukikwama mahali au ukihitaji ufafanuzi zaidi, usisite kuwasiliana nasi. Namba zetu zipo kwenye tovuti hii ukurasa wa mawasiliano. Pia tutaendelea kutoa mafunzo kuhusu Digital Marketing kupitia mfululizo wa makala zetu za Kiswahili na Kiingereza. 

Hitimisho

Digital Marketing ni habari njema kwa biashara za karne ya 21. Ni njia rahisi ya kujitangaza, kuuza na kujipatia wateja kwa urahisi. Mara nyingi unaweza kufanya bila hata gharama yoyote. Kwa wewe unayehitaji maarifa mapya yasiyo na ushindani mkubwa kwa sasa, jaribu hii fursa. Makala zinazofuata tutaelezea kiundani kuhusu mambo haya ambayo tumeyagusia kwa muhtasari.

Bofya HAPA kutazama huduma zetu au HAPA kuwasiliana nasi kama unataka kufahamu zaidi. Pia unaweza ku-share makala hii kwa mwingine.