Jinsi ya Kutengeneza M-Pesa Visa Card Nchini Tanzania
Hauhitaji tena Kwenda Bank kufungua akaunti ili upate kadi itakayokuwezesha kufanya malipo mtandaoni, hapa kikubwa una akaunti ya M-Pesa. Au unataka usitumie kadi yako ya CRDB/NMB kufanyia malipo mtandaoni?
Chukua simu yako, fuatilia makala hii itakayokusadia kufahamu jinsi ya kutengeneza Mpesa VISA card hatua kwa hatua na uzuri wake hakuna gharama yoyote utakayotozwa na haichukui zaidi ya dakika moja tayari unakuwa na kadi yako.
Kabla hatujaendelea tufahamu kwanza Mpesa visa kadi ni nini kwa undani wake.
M-Pesa Visa kadi ni nini?
Hii ni kadi mbadala ambayo humwezesha mtu kufanya malipo mtandaoni pindi anapokuwa ananunua bidhaa au huduma yoyote mtandaoni.
Kadi hii inaruhusu kutumia pesa zako zilizopo kwenye akaunti ya M-Pesa kufanya malipo yoyote ya kidigitali bila kuhamisha pesa Kwenda kwenye akaunti yako ya Bank.
M-Pesa Visa Kadi siyo kadi ya mkopo bali ni kadi ya malipo inayotengenezwa kupitia njia ya Mpesa tu yaani STK, USSD au App.
Baada ya kutengeneza M-Pesa Visa Kadi utapokea ujumbe wenye taaarifa zote kuhusu kadi yako ikiwemo kadi namba, tarehe itakayo-expire, CVV (Card Verification Value) namba.
Ili uweze kufanya malipo mtandaoni ni lazima uweke pesa kwenye kadi hiyo mara tu baada ya kuitengeneza au pale unapotaka kununua kitu.
CVV ni nini?
Baada ya kutengeneza kadi utatumiwa CVV namba, je CVV ni nini? Ni namba za usalama ambazo huwasaidia wamiliki wa tovuti kuhakiki kama kweli wewe ni mmiliki halali wa hiyo kadi, pia husadia kupunguza udanganyifu unaoweza kufanyika kutoka kwenye kadi yako ya M-Pesa.
Bila CVV namba huwezi kufanya muamala wowote ule. Namba hii pia inasimama kama nywila ya kadi yako unapotaka kununua kitu mtandaoni.
CVV zinafanya kazi ndani ya dakika 30 za mwanzo baada ya malipo kufanyika na hii husaidia kadi yako isitumiwe na mtu mwingine ambaye kwa bahati mbaya anaweza kujua taarifa za kadi yako na pia asiweze kubadilisha CVV namba. Hizo CVV zikishabadilishwa basi huwezi tena kuitumia hiyo kadi yako. Kuwa nazo makini.
Jinsi ya Kutengeneza M-Pesa Visa Kadi Nchini Tanzania.
Fuata hizi hatua kufanikisha zoezi hili,
- Bofya *150*00#.
- Chagua namba 4 LIPA kwa M-PESA.
- Chagua namba 6 M-Pesa VISA Card.
- Chagua namba 1 Tengeneza Kadi.
- Baada ya kufanikisha kutengeneza kadi, utapokea ujumbe wenye taarifa kuhusu kadi yako.
Jinsi ya Kuangalia Huduma Mbalimbali Kwenye Kadi Yako
- Bofya *150*00#.
- Chagua namba 4 LIPA kwa M-PESA.
- Chagua namba 6 M-Pesa VISA Card.
- Baada kuchagua namba sita utaona list ifuatayo (Tengeneza kadi. Taarifa za kadi. Weka Pesa kwenye Kadi. Salio la Kadi. Kadi Yangu. Msaada.)
Kwenye M-Pesa App
- Fungua M-PESA APP.
- Chagua Services tab.
- Chagua M-PESA Visa Card.
- Bofya Tengeneza M-PESA Visa Card.
- Baada ya hapo utapokea ujumbe wenye taarifa zako za kadi.
Utofauti wa Mpesa Visa card na MasterCard
Utofauti wake ni kwamba Mpesa Visa card inatumika kufanyia malipo mtandaoni tu, mwenye uwezo wa kuweka pesa (top up) kwenye hii card ni mmiliki pekee, huwezi kutumia kadi hii kwa lengo la kutumiwa pesa kutoka upande wa pili ikiwa MasterCard inaweza kutuma na kutumiwa pesa, kufanya malipo mtandaoni na mwisho kabisa card hii ni lazima iwe inashikika.
Mpesa visa card ni kwaajili ya malipo tu.
Huduma hii ya M-Pesa na Visa nchini Tanzania inaondoa kabisa haja ya kuwa na akaunti ya CRDB/NMB ili kufanya malipo mtandaoni kitaifa na kimataifa.
Kwa usalama zaidi, inashauriwa kurekodi maelezo ya kadi yako mahali salama na kufuta ujumbe wa nakala za Visa Kadi ya Mpesa kutoka kwenye Simu yako! ili kujiepusha kuvuja kwa taarifa zako za kadi.
Vodacom wamerahisisha maisha kwa kuweka uhusiano huu unaowawezesha watumiaji wa M-Pesa kufanya malipo kidigitali kupitia mtandao wa Visa wenye zaidi ya wafanyabiashara milioni 100.
Hivyo ndivyo unaweza kutengeneza M-Pesa Visa Card kwa ajili ya kufanya malipo yoyote mtandaoni.
Ahsante kwa kusoma Makala hii naitwa Anthony charles.