Kutaka Kuuza Leo Leo Kunagharimu Biashara Yako

Kutaka Kuuza Leo Leo Kunagharimu Biashara Yako

Takribani wiki mbili zilizopita nilipigiwa simu na mfanya biashara mmoja akisema nimsaidie kutengeneza website ambayo itampatia wateja pindi watakapotembelea website yake anasema yeye yuko tayari kulipa kiasi cha pesa ilimradi tu hayo matokeo anayoyataka ayaone. 

Nilijaribu kumwelekeza kuwa kwa upande wa website sisi tutafanya mikakati ya SEO kuifanya website yako ipande kwenye search engine ili mtu anapotafuta huduma unayoitoa aweze kukuona kirahisi kwenye search result ya google. Tutatoa mapendekezo maudhui yaweje kwenye website ili kuvutia zaidi. 

Baada ya hapo mtu hawezi kushawishika kununua huduma yako kwa kutembelea website yako tu kuna mambo mengi ambayo humfanya mteja afikie maamuzi ya kununua huduma yako ikiwemo maudhui yaliyopo kwenye website, muonekano wake lakini pia utofauti wako kwa social media (positioning). 

Sababu kwenye website kuna sehemu ambayo huwa tunaweka social media links mtembeleaji aki-click hizo link je huko kwenye social media atakuona kama ulivyojionyesha kwenye website? 

Je, marketing strategies zako zitamfanya mtu arudi tena kwenye website au ashawishike kununua bidhaa yako, brand yako ikoje? 

Website pekee haiwezi kukufanya upate wateja mtandaoni bali itakujengea visibility shikamavu mtandaoni.

Gharama ya kutaka kuuza leo leo

Mfanya biashara anakupatia fedha kwa mashart kweli kweli: “Nataka ndani ya mwezi huu nianze kuona matokeo, nipate wateja wa kutosha, followers wengi, I want to see big numbers n.k.” 

Ni kweli hakuna mtu ambaye anataka kutoa pesa yake halafu baadae asione matokeo. Hakuna. Kila mtu anataka kuona amepiga hatua kwenye kazi yake lakini ni vyema kujua ukweli kuhusu kupata wateja mtandaoni kabla hujaazimia kuanza kuuza bidhaa/huduma zako mtandaoni.

Hivyo inabidi ujue kuwa kuna mchakato hapa katikati mpaka kuwapata wanunuzi wa bidhaa yako ambao ni :

  1. Brand awareness (Watu wakufahamu)
  2. Build community (Watu wakuamini)
  3. Conversion (Watu wahamasike kununua)

Wengi wanakosea hapa:

Anarusha matangazo kwa media either yeye mwenyewe au marketers aliowalipa, akitarajia kupokea utitiri wa wateja. Lakini, asilimia 80 ya simu zinazopigwa zinaishia kwa watu kuuliza maswali kisha wanachikichia mitini. Kweli, idadi ya followers inaongezeka, lakini cha ajabu, mauzo hayaongezeki. 

Kwenye tangazo, comments zinasoma 500k hadi 800k, lakini matokeo anayoyatarajia yanagonga mwamba kila kukicha. Mteja anaanza kuwalaumu marketers kwa kushindwa kufikia matarajio yake.

Ikiwa anapata yote hayo, shida ni nini hasa?

Shida kubwa ni kwamba mfanya biashara anataka kuuza leo leo kupitia tangazo au matangazo mawili matatu aliyoyatengeneza jambo ambalo ni gumu kulifanikisha, hajui umuhimu na kujenga msingi thabiti kwenye mitandao ya kijami ili apate matokeo anayoyahitaji. 

Kuanza na malengo ya haraka bila kuwekeza katika brand awareness na kujenga community ni sawa na kujenga nyumba bila msingi imara. 

Watu wengi wanaweza kuona bidhaa yako, lakini kama hawakufahamu au hawana imani na brand yako, hawatachukua hatua ya kununua.

Matokeo hayo yanatokana na ukosefu wa uelewa kuhusu safari ya mteja (customer journey) na jinsi inavyohusiana na mauzo. 

Kwanza, ni muhimu kuhakikisha kuwa watu wanakufahamu (awareness), kisha wanakutambua na kukuamini (community building), na mwishowe wanakuwa tayari kununua (conversion). Hii ni safari inayohitaji muda, uvumilivu, na mikakati sahihi. 

Maudhui unayotengeneza leo yanaweza kukupa wateja wengine miezi sita ijayo. Jaribu kuliangalia soko kwa mwaka unaokuja utakuwa katika hali gani. 

Ni muhimu kujua mchakato mzima wa masoko utakaoupitia na nini kinachohitajika ili kufikia malengo yako ya kuuza mtandaoni kwa urahisi. 

Licha ya kuwa idadi ya followers ni muhimu, inapaswa kuwa na lengo la kujenga uhusiano wa muda mrefu na wateja kwanza ambao watahamasika kuja kununua bidhaa au huduma zako.

Mwisho

Kabla ya kurusha matangazo, ni vyema kuanza kwa kuwekeza muda na fedha katika kujenga brand awareness na community. 

Hii itahakikisha kwamba wanunuzi watakapokuwa tayari, tayari wamefahamu na kuamini brand yako, na wako tayari kuchukua hatua ya kununua. Mkakati huu wa hatua kwa hatua utaongeza uwezekano wa kupata matokeo ya kudumu, badala ya matokeo ya haraka yasiyo na msingi.

Mafanikio ya kweli kwenye masoko ya kidigitali hayaji bin vuu kwa usiku mmoja. Inahitaji uvumilivu na uwekezaji wa muda mrefu. 

Matokeo bora yanapatikana kwa kufuata hatua hizi muhimu na hatimaye utaona matokeo yanayodumu na yenye tija kwa biashara yako. 

LinkedIn ni Chuo: Umuhimu wa LinkedIn na LinkedIn Learning Katika Kujifunza. 

LinkedIn ni Chuo: Umuhimu wa LinkedIn na LinkedIn Learning Katika Kujifunza. 

LinkedIn ni chuo kilichosheheni walimu waliobobea kwenye fields zao. Ukiachana na kupost, ukitulia vizuri na ukaamua kujifunza kutoka kwa watu wengine, kuna vitu vingi utajifunza tofauti na mtu ambaye hayupo kabisa LinkedIn.

Kuna umuhimu mkubwa sana wa kutumia mtandao wa linkedIn mbali na kupost ama kutafuta kazi.

Wapo watu ambao yamkini hawajapata fursa yoyote lakini kuwepo kwao linkedin wamehamasika kubadili maisha na mitazamo yao kwa ujumla.

Binafsi SEO, personal branding na mambo ya marketing nimejifunza kupitia LinkedIn learning. Kuwepo linkedIn kumenisaidia sana katika career yangu.

Tuangalie umuhimu wa wewe kuwepo LinkedIn katika kujifunza.

1. Linkedin ni jukwaa la kujifunza na kukua kitaaluma.

LinkedIn ni tofauti na majukwaa mengine yalivyo. Hili jukwaa siyo tu la kuchapisha habari au kutafuta kazi; ni mahali pa kujenga connection, kunoa ujuzi, na kupata maarifa mapya kila siku.

Kupitia posts zako watu watakupongeza na kukuchallenge kuhusu taaluma yako jambo ambalo ni zuri katika kujifunza. Hii itakufungua ubongo ubadili mtazamo juu ya hicho unachokijua sasa.

Ukiona posts zako zinapata negative comment usiwaze sana ni mambo ya kawaida mtandaoni.

Pia LinkedIn inakupa uwezo wa kushirikiana na watu wenye ujuzi wa hali ya juu kitaaluma kukuzidi kwenye sekta mbalimbali, na kwa kusoma makala zao zenye kuelimisha unaongeza madini mapya yatakayokusaidia kukuza taaluma unayojishughulisha nayo. 

Cha kufanya chagua watu wako watano fuatilia makala zao kila siku, hudhuria event zao (virtual events), na shiriki kwenye posts zao hakika utaweza kufungua milango ya fursa nyingi ambazo huenda pengine usingezipata popote. 

2. Kujiendeleza kiujuzi kupitia linkedIn learning

LinkedIn pia ina sehemu muhimu sana inayoitwa LinkedIn Learning. Hiki ndicho kitu muhimu sana kwa kujifunza na ndiyo kitu kilinifanya niazimie kusema linkedin ni chuo. Iwe wewe ni mfanyabiashara, mhitimu, mfanyakazi au CEO, hii ni sehemu sawadata ya kujifunza maarifa mengi zaidi.

LinkedIn Learning ni jukwaa la mtandaoni lenye maelfu ya kozi zinazotolewa na wataalamu kutoka sehemu mbalimbali duniani. Uzuri wake ni kwamba kozi hizi zote zinatolewa bure kwa mwezi mmoja wa mwanzo. Jifunze jinsi ya kujiunga LinkedIn premium bure leo hii upate kufaidika na kozi zilizopo. 

Kupitia LinkedIn Learning, unaweza kujifunza kila kitu kutoka kwenye masuala ya teknolojia, biashara, uongozi, hadi kwenye ujuzi wa mawasiliano na usimamizi wa miradi. Faida kubwa ya kutumia LinkedIn Learning ni kwamba unaweza kujifunza kwa kasi yako mwenyewe, popote ulipo, na muda wowote.

3. Inakupa uhuru wa muda wa kujifunza. 

Hii inamaanisha kuwa hata kama una ratiba ngumu, bado unaweza kupata muda wa kuongeza maarifa na ujuzi mpya ambao utakuongezea thamani katika soko la ajira. Moja ya vitu vya kipekee kuhusu LinkedIn Learning ni kwamba kozi zake zimeundwa kwa namna ya kiutendaji. 

Badala ya kupata nadharia tu kama ilivyo chuoni, hapa unapata pia maarifa ya jinsi ya kutumia ujuzi huo katika hali halisi ya kazi ofisini kwako.

Hii inakusaidia si tu kujifunza bali pia kuwa na ujuzi unaohitajika kwenye nafasi yako ya kazi. Kwa mfano, kama unataka kuboresha ujuzi wako wa uongozi, unaweza kuchagua kozi zinazohusiana na uongozi na usimamizi, kisha ukajifunza mbinu mbalimbali zinazotumika kwenye mazingira halisi ya kikazi.

4. LinkedIn learning inatoa cheti kwa kila course. 

Zaidi ya hayo, unapomaliza kozi huko LinkedIn Learning unapewa cheti ambacho unaweza kuweka kwenye profile yako LinkedIn. Vyeti hivi vinaweza kuwa na uzito mkubwa, hasa unapojitambulisha kama mtu anayejali maendeleo ya kitaaluma na anayeendelea kujifunza kila mara.

Mfano ukiangalia profile yangu ya LinkedIn sehemu ya Certification and Licence utakuta kuna vyeti nilivyovipata linkedIn Learning nimeviambatanisha pale. Kwako vyeti hivyo vitaongeza mvuto wako kwa waajiri au wateja watarajiwa. 

Mwisho wa yote, LinkedIn Learning inathibitisha kwamba kujifunza hakuishii darasani pekee. Katika ulimwengu wa sasa wa kidigitali, ujuzi unapatikana popote, wakati wowote, na kupitia jukwaa kama LinkedIn, unaweza kufikia malengo yako ya kitaaluma na kuwa na mafanikio katika kazi na maisha yako kwa ujumla. 

Kwa hiyo, ikiwa unatafuta jukwaa la kujifunza, kuboresha ujuzi wako, na kuongeza thamani yako katika soko la ajira, LinkedIn Learning ni rasilimali muhimu sana ya kuchukua hatua hiyo.

Ajira Ni Tatizo: Fanya Mambo Haya Ukiwa Chuoni

Ajira Ni Tatizo: Fanya Mambo Haya Ukiwa Chuoni

Changamoto kubwa inayosumbua vijana wengi ni tatizo la ajira. Kila sehemu utasikia ajira hakuna ila kazi zipo.

Umekuwa wimbo unaovunja rekodi kila siku kuanzia juu hadi ngazi ya familia.

Wimbo huu unaongoza kwa kuimbwa na wahitimu wengi wa vyuo hapa nchini na kuna wengine wamegeuza tatizo hili kuwa fursa. Jambo ambalo ni zuri.

Ukiwa chuo usikae tu kizembe jaribu kufanya mambo mbalimbali yatakayokusaidia kukwepa Unemployment baada ya kumaliza chuo. Ni bora kujiandaa mapema kuliko kusubiri hatima usiyoijua.

Kukabiliana na janga hili kuhusu mbinu gani utumie kutafuta kazi, kwanza inabidi ujiulize wewe kama mwanafunzi unataka kuwa nani? Mpaka sasa unafanya nini kuhakikisha unakuja kuwa huyo mtu?

Chukua kalamu na karatasi narudia chukua karamu na karatasi sasa hivi kaa pembeni peke yako anza kuandika what is the person you really want to be in the future na huwezi kufikiria sawa sawa upate majibu ya maswali haya kwa kusoma tu lazima uandike kwenye karatasi ndio unapata kutambua kwa ufasaha majibu ya maswali hayo.

Vijana wengi husema acha kwanza nimalize itajulikana mbele kwa mbele. Mbele ipi wakati ukimaliza chuo unaenda kwenu ambako kupata fedha ya vocha tu ni changamoto!

Hivi unafikiri ukimaliza chuo mambo yatanyooka kama unavyotarajia? hata wao walifikiri vivyo hivyo kilichotokea hawaamini hadi leo.

Haya hapa mambo matano (5) ya kufanya ukiwa chuoni

1. Chagua kitengo/somo moja utakaloteseka nalo hadi kumaliza chuo.

Ukiwa chuo huwezi kuwa vizuri kwa yale yote yanayofundishwa darasani na pengine usiyafanyie kazi kabisa maishani mwako japo ni vizuri kuyafahamu.

Ukiamua kusoma course fulani chagua kitengo kimoja tu utakachokuwa unasoma kila siku iwe mchana iwe usiku unakomaa nacho mpaka unamaliza chuo mfano ukiamua kuchakalika na network hakikisha network haikupigi chenga, pata taarifa zote zinazohusu network.

Kuanzia mwaka wa kwanza hadi mwaka wa mwisho unakomaa na network ama kwa hakika utakuwa vizuri sana baada ya kumaliza chuo kuliko yule anayehangaika na vyote leo yupo Business management kesho hacking kesho kutwa Software development. Wahenga walisema mtaka yote kwa pupa hukosa yote.

Komaa na kitu kimoja, hayo masomo mengine yasome kwa ajili ya kunawilisha cheti chako. Hapa naomba tuelewane kitu unachokisoma hakikisha unalijua soko lake vizuri siyo unakomaa na hiki mwisho wa siku unaishia kufanya vitu tofauti kabisa.

 

2. Anza kujitolea mapema.

Usisubiri mpaka umalize chuo ndio uanze kutafuta sehemu ya kujitolea. Chuo ndio sehemu nzuri ya kujitolea ikiwa bado unapata fedha ya kujikimu kuliko ile unamaliza chuo ndio unajitolea yaani hata ukipewa pesa kidogo inaishia kununua dagaa na usafiri.

Fanya ufanyavyo ili mradi upate sehemu uanze kujitolea, kipindi unamaliza chuo pengine waweza kuajiriwa kwenye hiyo hiyo taasisi au kampuni kwa kuwa utakuwa tayari unajua ABC kuhusu mambo yanavyofanyika.

Kuna majukwaa pia ya kidigitali ambayo unaweza kujitolea kwenye makampuni ya nje ikiwa bado uko chuo kama vile SkilledUp Life hapa utatengeneza profile yako na kuapply kazi kulingana na field yako.  

Kipindi wenzako wanahangaika kutafuta kazi wewe utakuwa unahangaika kupanga mafaili. Ukijitolea mapema utapata uzoefu mapema utakaokusaidia baadae kujibu lile swali liuzwalo kwenye chumba cha usaili “una uzoefu wa miaka mingapi”.

3. Noa ujuzi wako kila siku.

Usitegemee tu kile unachofundishwa darasani. Mwanafunzi mzuri ni yule anayetaka kujua nyuma ya pazia pakoje.

Siku hizi kuna majukwaa mengi yatoayo kozi za bure na za kulipia mtandaoni ni wewe na bundle lako tu mfano YouTube hapa kuna kila aina ya kozi unayotaka kujifunza, kuna kila suluhu ya matatizo unayoyapitia.

Pia kuna LinkedIn Learning (Free & premium) na HubSpot Free Courses. Kozi zingine za bure uki-search tu google wanakuletea. Ujue kuna watu wengine wamejiajiri kwa kunoa juzi zao kupitia majukwaa haya haya! 

Usiseme huna bundle mbona ukiingia Insta au Tiktok unamaliza masaa mawili na ushee kutizama short videos? Bundle unalo sema bado hujaamua kuwa serious hebu kuwa serious uone kama utakosa pesa ya bundle.

Kama unataka kupata kubali kupoteza. Hakuna kitu cha bure duniani lazima ulipie.

4. Ishi Maisha yako.

Chuo kuna changamoto moja. Kila kijana anataka aonekane yeye ndio yeye si mtoto wa mkulima si mtoto wa Waziri si mtoto wa mfugaji wote wanataka kuishi maisha sawa.

Mwingine akipiga simu nyumbani laki mbili kwake ni pesa ya chai wakati kwako ni pesa ya kula miezi miwili hapo unalipa na kodi kabisa.

Lakini ukiwa chuo unataka uishi maisha sawa na wao. Fanya ujikubali, usiishi maisha ya kuigiza kumbuka maisha siyo kuigiza, fuata kilichokupeleka chuo hao marafiki unaoshinda nao leo siku mkimaliza chuo kila mtu ataenda kwao na wewe utaenda kwenu.

Kama huamini subiri mmalize chuo. Ukimpigia mwenzako atakwambia yuko ofisini utampigia baadae wakati wewe upo huko ndani ndani kwenye shamba la ndizi – Itaba.

Kama serikali inakulipia ada na umebahatika kupewa pesa ya kujikimu (BOOM) itumie vizuri pengine inaweza kukusaidia huko mbeleni.

5. Chagua marafiki wa kuishi nao.

Bwana mmoja alisema nikitaka kukujua wewe ni nani na mwelekeo wako ni upi nionyeshe marafiki zako watano. Nikiwaangalia marafiki zako basi nitapat kukujua wewe ni nani.

Kama wanapenda mitoko na wewe utakuwa nusu yake, kama wanapenda kusoma na wewe ni nusu yake, kama wanafanya biashara na wewe ni nusu yake, kama wanapenda kucheza PS na wewe ni nusu yake. 

Hebu angalia marafiki ulionao kwa sasa na mambo wanayoyafanya halafu angalia na yako kama yanatofautiana sana.

Kuwa na marafiki ambao hawaendi njia unayotaka Kwenda ni sawa na kujichimbia shimo la kujilaumu baadae.

Bora ujiengue mapema na haimaanisha uachane nao kabisa. Hapana.

Jiweke kando na fanya mambo kivyako vyako mkikutana sehemu bongeni kama hakuna lililotokea huku ukiwa na moja kichwani. Ukitaka kujua zaidi kasome kile kitabu cha ATOMIC HABIT by James Clear utaelewa zaidi ninachokwambia hapa.

Hao jamaa zako usiwachukie wala kujiona wewe ndio mwamba wa Lusaka, maisha siyo hivyo ishi nao kwa akili mana hao rafiki zako ndio wanaweza kukuletea michongo mingi endapo utakuwa na ujuzi zaidi kuwazidi wao.

Maisha ni watu ishi nao vizuri.

Chuo ni daraja tu unapita tumia muda mwingi kuifikirie sana kesho kuliko leo yako. Nimalize kwa kusema hakuna anayeijua kesho maisha yako yapo mikononi mwako.

Faida 5 za Kutumia Mtandao Wa LinkedIn Mbali na Kutafuta Kazi

Faida 5 za Kutumia Mtandao Wa LinkedIn Mbali na Kutafuta Kazi

Linkedin ni jukwaa lenye jumla ya watu wapatao milioni 950 kutoka nchi zaidi ya 200 ulimwenguni. Mtandao huu unakua kwa kasi sana kutokana na fursa mbalimbali ambazo watu wanapata hasa wanaotafuta kazi na wanaotangaza biashara zao.

Kuna faida gani za kutumia mtandao wa LinkedIn?  Katika makala hii nimeelezea faida tano za kutumia mtandao wa LinkedIn mbali na kutafuta kazi kama ilivyozoeleka kwa wengi.

Kujifunza.

Watu wengi wanajiunga LinkedIn kwa lengo la kutafuta kazi tu hasa vijana wanaomaliza vyuo, jambo ambalo linafanya baadhi yao kuja na mabango ya “Hi everyone, I am looking for new role and would appreciate your support. Thank you in Advance for any connection” baada ya hapo haonekani tena.

LinkedIn ni jukwaa linalokuwezesha wewe kujifunza mambo mengi yamkini hata yale uliyokuwa huyajui kutoka kwa wataalamu tofauti tofauti mfano HR, Engineer, Writers, Consultants, Career coach, Doctors, Marketers n.k wote hawa wako LinkedIn. 

Uzuri ni kwamba watu hawa hufundisha mambo kadha wa kadha ikiwemo mambo gani ufanye na yapi usifanye kulingana na tasnia zao. 

Mfano huko LinkedIn HR wanafundisha jinsi ya kujibu maswali ya interview ambayo mara nyingi watahiniwa huulizwa wakiwa kwenye chumba cha mahojiano (Interview)  kama vile “Unafikiri ni kwa nini wewe unafit kwenye hii kazi, tueleze wewe ni nani, tuulize swali kama una swali n.k”

Career Coach wanafundisha vitu ambavyo unatakiwa kujua kabla ya kwenda kwenye interview mfano “Jinsi ya kuelezea ujuzi wako, namna gani unaweza kuhama kutoka kitengo kimoja kwenda kitengo kingine bila kwenda kuongeza Masters wala kwenda kukisomea hicho kitu chuoni”.

Ukiachilia mbali hayo, LinkedIn learning inakupa free courses kwa mwezi mzima wa mwanzo baada kujiunga (kusubscribe) Linkedin Premium. Ofa hii ni kwa mwezi mmoja tu baada ya hapo utatakiwa kusitisha au kulipia ili uendelee na huduma (premium). 

Haya yote utajifunza huko huko LinkedIn, ni wewe na utayari wako wa kujifunza. 

Kuongeza marafiki wapya.

Marafiki hawa wanaweza kuwa ni wataalamu wanaokuzidi kimaarifa na kiujuzi, mnaendana au unawazidi kwa lengo la kubadilishana mawazo chanya katika tasnia zenu na pengine kufanya kazi pamoja. 

Mara nyingi urafiki huu waweza kukusaidia kutatua changamoto mbalimbali usizoweza iwe kwa kuongea nao kwenye simu, message, kusoma posts zao au kukutana nao sehemu ili kujadili zaidi baada ya kujuana.

Amini kwamba, milima haikutani lakini ninyi mnaweza kukutana katika namna ambao hukuitegemea, “aah! Kumbe ndo wewe sikutegemea kama tutakutana”. Leo mtakutana linkedIn kesho mtakutana Arusha live, uso kwa uso na huyo ndio anaweza kuwa mwenyeji wako. 

Leo mnaweza kuchati na kushiriki kwenye mijadala yenu pale LinkedIn lakini kesho inawezekana mkafanya kazi kwenye ofisi moja.

Kukuza Jina.

Kama hujulikani kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa, kitaifa basi LinkedIn inakupa fursa ya kujulikana siyo tu ngazi ya kitaifa bali ngazi za kimataifa. LinkedIn inakufungulia dunia kuwa unachotaka.

Huhitaji kukwea pipa mpaka marekani ili ujulikane unahitaji kuandaa maudhui yako yenye mvuto, yenye kutatua tatizo fulani, yenye kufundisha au yenye kuburudisha. Kwa kufanya hivi watu watapata kukujua wewe ni nani na unafanya nini.

Hivyo itakuwa rahisi kwako kupewa fursa za kazi kutokana na kile unachokiandika LinkedIn kwa sababu watu tayari watakuwa wanakujua. Hiyo ndiyo maana ya kukuza jina LinkedIn.

Watu hununua kwa watu wanaowajua. Vile watu hawaamini sana mitandao itakuchukua miezi hata mwaka mpaka watu waanze kukuamini na kukupa fursa au ufanye nao kazi. Kuza jina lako mtandaoni kwanza watu wakufaamu fursa za kazi zitakuja baadae. 

Kuwa mvumilivu milango ya fursa haifungukagi kizembe. Tia juhudi na nia matokeo utayaona mwenyewe.

Kukuza uandishi wako.

Baada ya kumaliza mtihani wa mwisho chuoni suala la kuandika huishia papo hapo. Pengine uandishi kwako ni changamoto sana je, ni sehemu gani unaweza kufanya mazoezi ya kujiendeleza kuandika au kufanya uandishi wako uwe umenyooka, fasaha?

Ukiniuliza mimi nitakwambia ni linkedin, kwa nini? Kwa sababu inakupa nafasi kubwa ya kuandika maneno mengi kadri uwezavyo, kuna sehemu ya posts na newsletter ambapo unaweza kuandika na kukuza uandishi wako siyo kama ilivyo X (Twitter).

Wengi hushindwa kujitosa na kiingereza chao cha you know kisa wataonekana si wasomi sana au utasikia ni vigumu sana kukaa na kuandaa maudhui kwa kuandika, practice makes more perfect anza hivyo hivyo mwisho wa siku mambo yatakaa mkao. Mchicha nao ulianza kama ua, mdogo mdogo unajifunza itafika wakati wewe mwenyewe utaoni kama mchezo tu.

Lengo la kuandika muda mwingine siyo uonekane unajua sana, au wewe ni smart sana lengo ni kufanya watu waelewe kwa urahisi kile unachokiwasilisha. Watu hawataki mambo magumu magumu be direct proportional kwa unachokipost.

Ikumbukwe: Mipaka ya lugha yako mipaka ya ulimwengu wako. Kingereza ni lugha ya kimataifa, kibiashara hivyo kwa namna yoyote ile inabidi uijue. 

Kutunza kumbukumbu. 

Nadhani ulishawahi kuweka kumbukumbu zako kwenye diary, notebook au kwenye application mbali mbali pia hata LinkedIn yaweza kutumika kwa miradi hiyo. Ukiweka post yako kule itakaa milele mpaka utakapoamua kuifuta mwenyewe.

Muda wowote waweza kuirejea, kujikumbushia au kutunza mawazo yako kule iwe kwenye post yako au kwa kuacha comment kwenye post za watu wengine.

LinkedIn is a note taking app.  

Mwisho, LinkedIn ni mtandao wenye faida kedekede hasa kwa mtu mmoja mmoja na kampuni kwa ujumla.

Usijifungie ghetoni au kukaa offline kisa hujapata kazi, ukiwa LinkedIn utajifunza mengi sana.

Jinsi ya Kutumia BOOM la Chuo Vizuri Kwa Manufaa Yako Baadae

Jinsi ya Kutumia BOOM la Chuo Vizuri Kwa Manufaa Yako Baadae

BOOM linatoka lini? Hili ni moja ya swali ambalo wanafunzi wanaodhaminiwa na serikali hujiuliza sana hasa wakati wanaanza shahada zao au pindi BOOM linapochelewa kutoka.

BOOM ni nini? 

BOOM ni fedha ya kujikimu inayotolewa na serikali kwa wanufaika wote wa mkopo kupitia Bodi ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu (HESLB -High Education Student’s Loans Board). 

Makato ya Mshahara baada ya kuajiriwa.

Wanafunzi wengi wamekuwa wakitumia fedha hiyo yamkini hata hawajui madhira watakayokuja kukutana nayo hapo mbeleni.

Hasa asilimia kumi na tano ya makato (15%) ya mshahara wao kutoka Bodi ya mikopo HESLB mara baada ya kuajiriwa, bado hujaweka NSSF, PSSSF, kodi ya nyumba, chakula n.k

Walioko maofisini wanaelewa vizuri athari za kukatwa kwa mshahara wao kila baada ya mwisho wa mwezi. Mshahara wa laki saba ukitoa makato makato unabakiwa na laki sita. Changamoto zingine pia huwa hazikosekani.

Ninachojaribu kusema ni kwamba ewe mwanafunzi uliyeko chuo na umebahatika kupata fedha ya kujikimu ali maarufu kwa jina la BOOM, itumie vizuri muda huu kwani kuna wengine hawapewi kabisa hiyo fedha, kila kukicha wanahangaika, leo kwa mjomba kesho kwa shangazi. 

Fedha hiyo inaweza kuwa msaada mkubwa katika maisha yako endapo utaitumia katika muktadha nzuri. 

Cha kusikitisha wengi huwa hatujali nini kitatokea huko mbeleni ilimradi tu umepata BOOM na maisha yanaenda. “Kula bata mpaka kuku aone wivu” ni sauti kutoka kwa vijana baadhi baada ya kupata BOOM.

Usishangae sana kuona mhitimu siku anamaliza chuo hata ile pesa ya kumrudisha nyumbani hana. Haya mambo yapo.

Kila mtu ana malengo yake chuoni, usiwe bendera kufuata upepo

Ndiyo, najua kila mtu chuoni huwa ana malengo yake, yawezekana kwao zipo, yupo chuo kukamilisha ngazi za elimu. Je, wewe kijana mwenzangu kutoka ndani ndani huko Ifunde unataka uishi kama wao!.  

Kuna maana gani ya kununua rundo la nguo, nguo za bei ghari wakati hata maarifa ya kukusaidia kuiishi kesho yako huna? Ni kwa kuwa BOOM limetoka au ni kwa sababu marafiki zako wanafanya hivyo?.

Wengine wanashindana kuvaa vizuri, kutafuta pisi kali (msichana) kisa wamepata BOOM. Jiulize, mpaka sasa umefanya nini cha maana kutokana na hilo BOOM unalopewa?

Kumbuka chuo ni daraja tu unapita, bado una safari ndefu ya kutembea na inawezekana hao vijana wenzako unaokula nao bata chuoni usiwaone tena katika maisha yako. Usiwe bendera kufuata upepo.

Wakati mwingine huwa ni vigumu sana kwenda kinyume na marafiki zako uliozoeana nao toka mwanzo. Lakini ukweli ni kwamba mwisho wa siku kila mtu atashika njia yake. 

Chaguo ni lako uishi maisha ya kuigiza ili uendane na wenzako au ukubali kuishi maisha yako – ujikubali. Kingine, usiangalie tu miaka utakayokuwepo chuoni bali miaka baada ya kumaliza chuo.

BOOM ni mtaji. 

Kama wewe ni kijana kutoka familia ya wakulima, Boom ni fedha unayoweza kuitumia kuwekeza katika kilimo, kununua ardhi, ufugaji au kuwasaidia wazazi wako kuliko kula bata chuoni. 

Kununua vifaa mbalimbali vitakavyokupa sehemu ya kuanzia baada ya kumaliza chuo mfano computer, kamera, vifaa vya stationary n.k. 

Jifunze maarifa mapya mtandaoni yatakayokuongezea ujuzi wa kile unachokisomea kuliko kuchoma pesa kwa ajili ya kuangalia short videos Tiktok. 

Kuanzisha biashara ndogo ndogo kama kuuza karanga, vifaa vya kieletroniki, nguo au chochote kitakachokuwa ndani ya uwezo wako, maarifa utakayoyapata hapa ni sawa na mtu anayefanya internship kwenye kampuni fulani.   

Hujawahi kuona mwanachuo anauza karanga, popcorn, simu + covers? Naam, tumia BOOM katika miradi hiyo. 

Siku njema huonekana asubuhi.