Ajira Ni Tatizo: Fanya Mambo Haya Ukiwa Chuoni

Written by Anthony Charles

Anthony Charles is a young Web Designer and Developer | Content Writer. Helping Individuals escape unemployment, SMEs grow their visibility online.

Posted March 24, 2024

Changamoto kubwa inayosumbua vijana wengi ni tatizo la ajira. Kila sehemu utasikia ajira hakuna ila kazi zipo.

Umekuwa wimbo unaovunja rekodi kila siku kuanzia juu hadi ngazi ya familia.

Wimbo huu unaongoza kwa kuimbwa na wahitimu wengi wa vyuo hapa nchini na kuna wengine wamegeuza tatizo hili kuwa ajira. Jambo ambalo ni zuri.

Ukiwa chuo usikae tu kizembe jaribu kufanya mambo mbalimbali yatakayokusaidia kukwepa Unemployment baada ya kumaliza chuo. Ni bora kujiandaa mapema kuliko kusubiri hatima usiyoijua.

Kukabiliana na janga hili kuhusu mbinu gani utumia kutafuta kazi, kwanza inabidi ujiulize wewe kama mwanafunzi unataka kuwa nani? Mpaka sasa unafanya nini kuhakikisha unakuja kuwa huyo mtu?

Vijana wengi husema acha kwanza nimalize itajulikana mbele kwa mbele. Mbele ipi wakati ukimaliza chuo unaenda kwenu ambako kupata fedha ya vocha tu ni changamoto!

Hivi unafikiri ukimaliza chuo mambo yatanyooka kama unavyotarajia? hata wao walifikiri vivyo hivyo kilichotokea hawaamini hadi leo.

Haya hapa mambo matano (5) ya kufanya ukiwa chuoni

1. Chagua somo moja utakaloteseka nalo hadi kumaliza chuo.

Ukiwa chuo huwezi kuwa vizuri kwa yale yote yanayofundishwa darasani na pengine usiyafanyie kazi kabisa maishani mwako japo ni vizuri kuyafahamu.

Ukiamua kusoma course fulani chagua kitengo kimoja tu utakachokuwa unasoma kila siku iwe mchana iwe usiku unakomaa nacho mpaka unamaliza chuo mfano ukiamua kuchakalika na network hakikisha network haikupigi chenga, pata taarifa zote zinazohusu network.

Kuanzia mwaka wa kwanza hadi mwaka wa mwisho unakomaa na network ama kwa hakika utakuwa vizuri sana baada ya kumaliza chuo kuliko yule anayehangaika na vyote leo yupo Business management kesho hacking kesho kutwa Software development. Wahenga walisema mtaka yote kwa pupa hukosa yote.

Komaa na kitu kimoja, hayo masomo mengine yasome kwa ajili ya kunawilisha cheti chako.

ALSO READ:  Jinsi Nilivyopata Mteja Linkedin Nikiwa Bado Mwanafunzi

 

2. Anza kujitolea mapema.

Usisubiri mpaka umalize chuo ndio uanze kutafuta sehemu ya kujitolea. Chuo ndio sehemu nzuri ya kujitolea ikiwa bado unapata fedha ya kujikimu kuliko ile unamaliza chuo ndio unajitolea yaani hata ukipewa pesa kidogo inaishia kununua dagaa na usafiri.

Fanya ufanyavyo ili mradi upate sehemu uanze kujitolea katika kipindi unamaliza chuo pengine waweza kuajiriwa kwenye hiyo taasisi au kampuni kwa kuwa utakuwa tayari unajua ABC kuhusu mambo yanavyofanyika.

Kuna majukwaa pia ya kidigitali ambayo unaweza kujitolea kwenye makampuni ya nje ikiwa bado uko chuo kama vile SkilledUp Life hapa utatengeneza profile yako na kuapply kazi kulingana na field yako.  

Kipindi wenzako wanahangaika kutafuta kazi wewe unahangaika kupanga mafaili. Ukijitolea mapema utapata uzoefu mkubwa utakaokusaidia baadae kujibu lile swali liuzwalo kwenye chumba cha usaili “una uzoefu wa miaka mingapi”.

3. Noa ujuzi wako kila siku.

Usitegemee tu kile unachofundishwa darasani. Mwanafunzi mzuri ni yule anayetaka kujua nyuma ya pazia pakoje.

Siku hizi kuna majukwaa mengi yatoayo kozi za bure na za kulipia mtandaoni ni wewe na bundle lako tu mfano YouTube hapa kuna kila aina ya kozi unayotaka kujifunza, kuna kila suluhu ya matatizo unayoyapitia.

Pia kuna LinkedIn Learning (Free & premium) na HubSpot Free Courses. Kozi zingine za bure uki-search tu google wanakuletea. Ujue kuna watu wengine wamejiajiri kwa kunoa juzi zao kupitia majukwaa haya haya! 

Usiseme huna bundle mbona ukiingia Insta au Tiktok unamaliza masaa mawili na ushee kutizama short videos? Bundle unalo sema bado hujaamua kuwa serious hebu kuwa serious uone kama utakosa pesa ya bundle.

Kama unataka kupata kubali kupoteza. Hakuna kitu cha bure duniani lazima ulipie.

4. Ishi Maisha yako.

Chuo kuna changamoto moja. Kila kijana anataka aonekane yeye ndio yeye si mtoto wa mkulima si mtoto wa Waziri si mtoto wa mfugaji wote wanataka kuishi sawa.

ALSO READ:  Usalama Mtandaoni ni nini? Umuhimu na Jinsi Ya Kuwa Salama.

Mwingine akipiga simu nyumbani laki mbili kwake ni pesa ya chai wakati kwako ni pesa ya kula miezi miwili na hapo unalipa na kodi kabisa.

Lakini ukiwa chuo unataka uishi maisha sawa na wao. Fanya ujikubali, usiishi maisha ya kuigiza kumbuka maisha siyo kuigiza, fuata kilichokupeleka chuo hao marafiki unaoshinda nao leo siku mkimaliza chuo kila mtu ataenda kwao na wewe utaenda kwenu.

Kama serikali inakulipia ada na umebahatika kupewa pesa ya kujikimu (BOOM) itumie vizuri pengine inaweza kukusaidia huko mbeleni.

5. Chagua marafiki wa kuishi nao.

Bwana mmoja alisema nikitaka kukujua wewe ni nani na mwelekeo wako ni upi nionyeshe marafiki zako watano kwamba hao marafiki ni nusu ya wewe.

Kama wanapenda mitoko na wewe utakuwa nusu yake, kama wanapenda kusoma na wewe ni nusu yake, kama wanafanya biashara na wewe ni nusu yake, kama wanapenda kucheza PS na wewe ni nusu yake. 

Hebu angalia marafiki ulionao na mambo wanayoyafanya halafu angalia na yako kama yanatofautiana sana.

Kuwa na marafiki ambao hawaendi njia unayotaka Kwenda ni sawa na kujichimbia shimo la kujilaumu baadae.

Bora ujiengue mapema na haimaanisha uachane nao kabisa. Hapana.

Jiweke kando na fanya mambo kivyako vyako mkikutana sehemu bongeni kama hakuna lililotokea huku ukiwa na moja kichwani.

Usiwachukie wala kujiona wewe ndio mwamba wa Lusaka, maisha siyo hivyo ishi nao kwa akili mana hao rafiki zako ndio wanaweza kukuletea michongo mingi endapo utakuwa na ujuzi zaidi kuwazidi wao.

Chuo ni daraja tu unapita tumia muda mwingi kuifikirie sana kesho kuliko leo yako. Nimalize kwa kusema hakuna anayeijua kesho maisha yako yapo mikononi mwako.

0 Comments

Submit a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

You May Also Like

Products From Tanzlite