Mara nyingi umekuwa ukisikia watu wanaongelea kuhusu fursa unazoweza kufanya kupitia majukwaa ya kidigitali lakini bado hujajua hizo fursa ni zipi, na unawezaje kuzipata? Kwenye makala hii nitakuelezea kwa ukaribu hizo fursa, namna ya kuzipata na jinsi ya kuzitumia ili kujiingizia kipato.
Majukwaa ya kidigitali yamekufungulia dunia kuwa unachotaka, fursa zote unazo kiganjani mwako. Unaweza kufanya biashara yako binafsi kupitia hii hii mitandao na kujipatia kipato au kufanya kazi na mtu yeyote kutoka sehemu mbalimbali bila kuonana uso kwa uso.
Kitu chochote unachoweza kufanya kidigitali na kikakuletea faida hiyo ni fursa.
Mfano, Natoa huduma za kupamba kumbi za sherehe, nitaanza kushare picha zikinionyesha napamba kumbi mbalimbali kwa ajili ya sherehe tofauti kama harusi, mikutano, sendoff au kitchen party ili atakayeona na kuvutiwa anitafute tufanye kazi.
Hivyo ndio jinsi fursa za kidijitali zilivyo kuuza ujuzi au bidhaa zako mtandaoni kwa watu wengi kwa mara moja. Kuna Aina nyingi za Fursa mtandaoni ni wewe tu kuchagua ipi itakufaa
1.Kuuza Huduma zako(Services)
Hii inaweza kuwa huduma unayoitoa wewe mwenyewe binafsi au kama kampuni. Mfano kufundisha au kusherehesha. Dukahuru anapatikana Instagram akifundisha watu wengine jinsi ya kuuza bidhaa mtandaoni na huduma nyingine nyingi.
Kama wewe unaweza kufanya hivyo basi hiyo ni fursa ikimbilie mapema.
Huduma ya kikampuni ni kama ile anayofanya Haika Lawere anakodisha kumbi zake kwaajili ya sherehe, vikao au makongamano. Pale instagram huwa anapost picha za kumbi, bei na mawasiliano kwa atakayehitaji.
Wewe kijana au wewe ndugu yangu uliye kwenye kampuni na una matazamio ya kupata chochote kutokana na hilo kampuni unalofanyia kazi, tumia muda huo kuji-promote kwa kutumia status ya kampuni ili hata siku umetoka, utoke na jina.
Kwa yule mwenye uwezo wa kufanya kama Haika basi fanya, hiyo pia ni fursa itakayofanya usihangaike kutafuta fursa zingine.
2.Kuuza bidhaa zako binafsi (Products)
Mfano; unamiliki duka la kuuza mafuta ya nywele, una simu janja, jiunge mtandao wa Instagram, fungua kurasa yako na anza kupost mafuta yako unayouza, kumbuka jinsi utakavyojinadi katika bidhaa yako ndivyo utakavyoweza kupata wateja.
Hapa nazungumzia jinsi ya kupost(maudhui). Watu mbalimbali wataona bidhaa yako na watakutafuta ili hali uliweka mawasiliano kwenye kurasa yako.
Je, ushawahi kununua kitu mtandaoni? Kama jibu ni ndiyo basi hata wewe unaweza kuuza kitu chochote mtandaoni. Unahitaji tu kujua wateja wako wanapatikana mtandao upi, jifunze jinsi ya kutumia mtandao husika vizuri na upeleke biashara yako huko.
3.Kuuza bidhaa za watu wengine (Affiliate Marketing)
Kama hauna mtaji wa kuanzishia biashara yako na hauna biashara yoyote unayoifanya. Tafuta kampuni au biashara ya mtu ambaye utakuwa unamsaidia kutafuta wateja mtandaoni au kufanya biashara yake ijulikane kwa watu wengi.
Mtu anayefanya kazi ya affiliate marketing hulipwa kutokana na mauzo yatokanayo na juhudi zake za kuleta wateja. Hii unaweza kuifanya kwenye blog, tovuti yako binafsi au kwenye mitandao ya kijamii.
Pia kuna makampuni yana bidhaa zao na yanatafuta watu wa kuwasaidia kuuza au kuwafikia wateja na kwa kila mteja utakayemleta utapewa Kamisheni.
Kamisheni ndo itakua faida yake kutokana na makubaliano mtakayoweka.
4.Kushawishi watu kununua bidhaa Fulani (Influencing)
Hii inatumiwa sana na makampuni mbalimbali makubwa na madogo. Kutafuta watu wenye ushawishi mtandaoni kuweza kushawishi watu watumie huduma au bidhaa zao. Na utalipwa kwa makubaliano mtakayoweka. Mfano Lilian Lema anafanya hii kazi Instagram na kulipwa.
Utahitaji kuwa na page yako ambayo umeijenga mwenyewe na kupata wafuasi ambao utaweza kuwashawishi. Sio lazima uanze ushawishi kwa kulipwa unaweza fanya bure na badae ukaanza kuchaji watu wakitaka huduma hiyo kwako.
Hili ndo somo langu la leo kuhusu fursa za kidigitali, haimaanishi ndio mwisho wa fursa, Hapana. Kutokana na hizo nne unaweza pata fursa nyingine zaidi. Muhimu ni kujiamini unaweza na kuanza kufanya.
Hauhitaji tena Kwenda Bank kufungua akaunti ili upate kadi itakayokuwezesha kufanya malipo mtandaoni, ili mradi tu una akaunti ya M-Pesa. Au una kadi yako ya CRDB/NMB lakini hutaki kuitumia kufanyia malipo mtandaoni?
Chukua simu yako, tengeneza VISA Kadi leo kwani hakuna gharama yoyote utakayotozwa na haichukui zaidi ya dakika moja unakuwa tayari una kadi yako.
M-Pesa Visa Kadi ni nini?
Hii ni kadi mbadala ambayo humwezesha mtu kufanya malipo mtandaoni pindi anapokuwa ananunua bidhaa au huduma kwa kutumia akaunti yake ya M-Pesa.
Kadi hii inaruhusu kutumia pesa zako zilizopo M-Pesa kufanya malipo yoyote ya kigitali bila hata ya kuhamisha pesa Kwenda Bank.
M-Pesa Visa Kadi siyo kadi ya mkopo bali ni kadi ya malipo inayotengenezwa kupitia njia ya Mpesa yaani STK, USSD au App.
Baada ya kutengeneza M-Pesa Visa Kadi utapokea ujumbe wenye taaarifa zote kuhusu kadi yako ikiwemo kadi namba, tarehe itakayo-expire, CVV (Card Verification Value) namba.
Ili uweze kufanya malipo mtandaoni ni lazima uweke pesa kwenye kadi yako mara tu baada ya kuitengeneza au pale unapotaka kununua kitu.
CVV ni nini?
CVV ni namba za usalama ambazo huwasaidia wamiliki wa tovuti kuhakiki kama kweli wewe ni mmiliki halali wa hiyo kadi, pia husadia kupunguza udanganyifu unaoweza kufanyika kutoka kwenye kadi yako ya M-Pesa.
CVV zinafanya kazi ndani ya dakika 30 za mwanzo baada ya kufanya malipo. Hii husaidia kadi yako isitumiwe na mtu mwingine ambaye kwa bahati mbaya anaweza kujua taarifa za kadi yako na pia asiweze kubadilisha CVV namba. Hizo CVV zikishabadilishwa basi huwezi tena kuitumia hiyo kadi yako. Kuwa nazo makini.
Jinsi ya Kutengeneza M-Pesa Visa Kadi Nchini Tanzania.
Fuata hizi hatua kufanikisha zoezi hili,
Bofya *150*00#.
Chagua namba 4 LIPA kwa M-PESA.
Chagua namba 6 M-Pesa VISA Card.
Chagua namba 1 Tengeneza Kadi.
Baada ya kufanikisha kutengeneza kadi, utapokea ujumbe wenye taarifa kuhusu kadi yako.
Jinsi ya Kuangalia Huduma Mbalimbali Kwenye Kadi Yako
Bofya *150*00#.
Chagua namba 4 LIPA kwa M-PESA.
Chagua namba 6 M-Pesa VISA Card.
Baada kuchagua namba sita utaona list ifuatayo (Tengeneza kadi. Taarifa za kadi. Weka Pesa kwenye Kadi. Salio la Kadi. Kadi Yangu. Msaada.)
Kwenye M-Pesa App
Fungua M-PESA APP.
Chagua Services tab.
Chagua M-PESA Visa Card.
Bofya Tengeneza M-PESA Visa Card.
Baada ya hapo utapokea ujumbe wenye taarifa zako za kadi.
Huduma hii ya M-Pesa na Visa nchini Tanzania inaondoa kabisa haja ya kuwa na akaunti ya benki ili kuwa na kadi, na hivyo kufanya malipo kimataifa.
Kwa usalama zaidi, inashauriwa kurekodi maelezo ya kadi yako mahali salama na kufuta ujumbe wa nakala za Visa Kadi ya Mpesa kutoka kwenye Simu yako!
M-Pesa inaweza kupanua mtandao wake ikiwa na Visa. Ushirikiano huu utawawezesha watumiaji wa M-Pesa kufanya malipo ya kidijitali kupitia mtandao wa Visa wenye zaidi ya wafanyabiashara milioni 100. Awali, watumiaji wa M-Pesa walikuwa wamezuiliwa kufanya malipo ndani ya mtandao wa wafanyabiashara kwa mfumo wa M-Pesa.
Ushirikiano wa M-Pesa na Visa unaweza kuongeza matumizi ya mfumo huo kwa kutoa mtandao mpana wa ununuzi kwa watumiaji, ambao pia husaidia kuongeza uwezo wa mapato ya mfumo.
Ahsante kwa kusoma Makala hii.
Naitwa Anthony charles Mwandishi katika makala za Tanzlite.
Haijarishi kuwa wewe ni mtoto wa mkulima, huna connection, umetafuta kazi umekosa, watu hawakujui au upo kwenye harakati za kujitafuta. Chukua simu yako zama mtandaoni huko ndiko fursa zilipo.
The universal does not belong to anyone group of people, everyone story is potentially universal it just need to be told well by Chimamanda Adichie
Tupo kwenye ulimwengu wa kidigitali ambao kila mmoja wetu anatumia mitandao ya kijamii kama Linkedin, Twitter, Instagram na Facebook ambapo kuna uwezekano mkubwa wa kujipenyeza nakujenga jina katika majukwaa hayo.
Imebaki kwako, kama Joti anajulikana kwa kuchekesha, wewe utajulikana katika lipi?
Kuna umuhimu gani wa kujenga jina mtandaoni?
Swali zuri, hautengenezi jina peke yake bali unajitengenezea mazingira mazuri ya kuondokana na kile wanachokiita unemployment na kuwa kwenye uwanja mzuri wa wajasiriamali.
Uwanja ambao hata kama baadae ukija kuanzisha biashara yako iwe ni rahisi kuaminiwa na kupata wateja kwa urahisi.
Kutengeneza jina mtandaoni ni sawa na kuwa na bima ambayo itakusaidia wewe usihangaikei pindi mambo yatakapoenda ndivyo sivyo.
Saivi ni kawaida mtu kumaliza chuo na kurudi nyumbani kwenda kulima viazi, mwajiriwa kuendelea kutegemea mshahara, kuendelea kujitolea kwa sababu hakuna namna nyingine itakayomfanya apate pesa.
Ulishawahi kusikia watu wanafanya kazi kama freelancer, yaani mtu aliyeko Washington Dc anampa kazi mtu aliyeko Tanzania? Huko ndiko kuzisaka fursa mtandaoni.
Unaikumbuka hii sauti “Tunakufungulia dunia kuwa unachotaka” au “Dunia ipo kiganjani mwako”
Ni njia zipi zitakazokusaidia kujenga na kukuza jina mtandaoni?
Unataka kuwa nani?
Hata nchi yenyewe huwa inaweka malengo ya muda mrefu na ya muda mfupi. Pasipo malengo ni sawa na kuendesha gari huku umesinzia.
Kama tayari unajua baada ya miaka mitano unataka kuwa mtu fulani ni vizuri zaidi na kama bado hujajua chukua kalamu yako, andika malengo yako pembeni, njia hizo zisipo fanya kazi basi jitafute mpaka ujipate. Mali bila daftari huisha bila kujua.
Je kweli umeandika? Hii itakusaidia pale unapoanza kukuza jina lako mtandaoni kwa kuangalia zaidi malengo yako yanasemaje, isije ikawa unatwanga maji kwenye kinu.
Unataka ujulikane katika lipi?
Watu wakianza kusema napenda unavyoongea, napenda idea zako n.k maana yake umeweza kujitofautisha na wengine.
Ukisikia diamond, Patrick lumumba amearikwa kwenye tamasha, unafikiri ni nini kitaenda kufanyika? Vipi ukisikia Elon Musk, Steve Job au putin?.
Najua unachokifikiria saivi lakini hivyo ndivyo inabidi ujulikane katika mitandao, inakuwa ni rahisi watu kukujua na kukufuatilia. Mtu akiona tu profile yako anajua huyu ni fulani anazungumzia vitu fulani, simple like that.
NB: Hapa kidogo inahitaji juhudi na uvumilivu kwa sababu mwanzoni utahangaika sana, hakuna likes, hakuna comment yoyote, hakuna mtu anayeonekana kukusupport lakini kumbuka malengo yako yanasemaje na endelea kusonga mbele. Kitu kizuri lazima ukihangaikie. Ukweli ni kwamba watu wanaona na kusoma post zako kila siku.
Ni mitandao ipi uwepo?
Kulingana na malengo yako chagua majukwaa yasiyozidi matatu ili uwe na uwezo wa kuyahimili mfano Linkedin, Youtube, Twitter, Instagram.
Kukuza jina katika majukwaa haya kama nilivyo sema ni shughuli kidogo inakubidi ujitume kuwa active, onyeshe uhai wako kwa kupost, kushiriki kwenye post za watu wengine. Jinsi watu wanavyoona profile yako kila siku ndivyo wanavyozidi kukumbuka.
Ni maudhui gani upost?
Post chochote kama profile yako inavyojieleza hakikisha post zako ziwe kwenye mazungumzo yaani mtu akiwa anasoma awe kama vile anaongea na wewe tofauti na hapo post zako zitaonekana zimeandikwa na Chatgpt, hazina mguso.
Hakikisha unatumia style mbali mbali katika kuwasilisha maudhui yako ili usiwachoshe wasomaji mfano tumia image, graphics, texts au short video kama ni itakupendeza.
Kitu kinachokufanya uonekane tofauti na wengine ni historia yako pamoja na vitu unavyovifanya katika hadhara ya mamilioni ya watu, wataalamu wa sales and marketing wanasema ujiuze.
Social media is indeed the best way to build an audience as it’s reach is global and connecting is as easy as few clicks ~ Jules Marcoux
Post yako lazima iwe
Inalenga mtu au kundi fulani la watu
Inatatua changamoto fulani
Inaelimisha jambo fulani na
Siyo, from no where umekula zako sangala unaenda kujipost.
Fahamu hadhira yako.
Watu wote mtandaoni hawawezi kuwa hadhira yako, ni lazima uchague aina fulani ya watu ambao ndiyo target yako. Mtandaoni kuna watu wa kila aina, siyo lazima kila mtu akujue okay! au wewe umewahi kwenda kununua nguo buchani?
Kujenga jina maana yake ni kujenga mahusiano mazuri na watu unaowalenga, watakao furahia uwepo wako na walioko tayari kupokea kile utakachowapatia.
Watu hununua bidhaa au maarifa kutoka kwa watu wanaowajua na kuwaamini. Soko ni watu na watu wako mtandaoni, wafuate huko huko waliko.
Ni matumaini yangu umejifunza kitu. Ahsante ndugu.
Je, mitandao inakutumia zaidi kuliko unavyotakiwa kuitumia?. Leo hii mtu akinunua simu kubwa (smartphone) kitu cha kwanza anachokimbilia ni kujipost mtandaoni hata kama yuko kitandani, je hivi ndivyo tunavyotakiwa tuitumie mitandao?
Kuwa kwenye ulimwengu wa kidigitali kunafanya watu wengi washindwe kuzikabili hisia zao. Pia wengi hawana uelewa kuhusu namna nzuri ya kuitumia mitandao hii.
Unajipost kila siku mtandaoni, unaeleza hisia zako kuhusu wewe angali bado kijana ambaye hujui hata kesho yako itakuwaje. Picha isiyo na maadili ukishaipost mtandaoni hiyo imeenda, watu wataiona na itahifadhiwa kwenye algorithms.
Basi, hata kama unajipost hakikisha hiyo picha inatunza heshima yako na inaleta mantiki kwa mtu yeyote. Muda huo angalau jifunze skills zitakazokusaidia kutengeneza ajira yako mwenyewe.
Mfano, Tuseme kampuni fulani inataka ikuajiri je, ikiangalia picha zako mtandaoni utafaa kweli kupewa hiyo kazi? Kwa sababu jinsi unavyojipost ndivyo unavyojielezea zaidi kuwa wewe ni nani, ni wa aina gani, unafanya nini, unapenda nini, uko makini kiasi gani?
Picha zako mtandaoni ni ushahidi tosha watu kukujua vizuri kuliko unavyojijua.
Mitandao ni sehemu ambayo unaweza kutafuta kupata fursa, kujifunza maarifa mbali mbali kutoka kwa watu wengine.
Itumie mitandao katika miradi hiyo na si kuvimbiana au kujionyesha kana kwamba upo kwenye maonyesho.
Ndiyo maana ni ngumu sana vijana kutoboa kupitia mitandao ya kijamii. Ukiangalia wanigeria au wakenya wanakimbiza soko kimataifa kupitia hii hii mitandao.
Ziko wapi ajira? Ni sauti ya kila kijana baada ya kuhitimu chuo. Mitandao ni fursa shituka, tangaza kitu kinacholeta mantiki kwa watu usitangaze hisia zako.
Unaweka nini kwenye akili za watu pale wanapoona ulichokipost? Ifikie mahari uwe na fikra za mbali baada ya miaka mitano mbele, kile ulichokipost kitakutambulisha kama nani?
Tunaishi kwenye ulimwengu wa kidigitali ambao mtu anaweza kufanya kazi remotely, itafika muda baadhi ya ajira kama siyo zote zitakuwa zinatolewa baada ya waajiri kukuona mtandaoni unafanya kitu fulani ambacho wanauhitaji nacho.
Soko la kimataifa linahitaji watu wanaoweza kufanya kazi kama freelancer (mtendaji huria).
Na atakayepata bahati hii ni yule ambae account zake za mitandao ya kijamii inajieleza yenyewe vizuri kuhusu yeye, na yuko active. Hakuna kutuma maombi wala interview labda iwe ni lazima. Mtu huyu atashuhudia message ikiingia au akipigiwa simu zikisema
Habari,
Nimekuona kwenye mitandaoni ukielezea zaidi kuhusu blablaa ah! nimekuwa nikikufuatilia toka muda …, vipi unaweza kunisaidia kufanya hili jambo fulani?
Noah Harari Alisema “We are going to believe more on algorithms than we believe in ourselves”.
Japo watu wengi hawajui ni kwa namna gani google hacking inaweza kutumika kupata taarifa zako nyeti binafsi, ni kwa namna gani active attack inaweza kufanyika kwa mtu binafsi au kwenye taasisi?. Na kibaya zaidi watu wengi hawaamini haya mambo utasikia, hii technolojia bado sana kwetu, nani atani-hack mimi wakati hata pesa sina? Ni sawa lakini haya pia yanaweza kutokea.
Tabia ya kupost maisha yako au familia yako kwenye mitandao siyo nzuri na inaweza kukugharimu baadae.
Si kuna watu wanasoma cybersecurity nchi hii, subiri baada ya miaka mitano tutakuwa na vijana wengi ambao hawana ajira na kazi yao itakuwa ndiyo hiyo KUHACK.
Tumia mitandao ya kijamii katika namna ambayo haitakuja kuharibu heshima yako. Ahsante ndugu.
Kila sehemu AI, AI, AI inaenda kuchukua nafasi za wale wanaocode (Developers). Hata kipindi google inaanza watu walitabiri kuwa developers wengi watakosa kazi.
Je, developers walikosa kazi? AI ni kama google tu. Kwa nini uogope wakati maendeleo ya sayansi na technolojia yanaibua fursa zingine mpya ambapo developers wanahitajika ili kurahisisha zaidi maisha ya watu waendane na ulimwengu wa IoT?
Mfano. Mobile Application (siku hizi kila mtu anasimu), Integrated secured system (kuunganisha mifumo miwili Mfano, idara ya maji na TRA), IoT (Internt of Things), software, web based system na zingine nyingi zinazotatua changamoto mbalimbali kwenye jamii.
AI yupo anaweza kunisaidia kufanya vyote hivyo
Ndiyo, lakini kama huna ujuzi wa kucode huwezi fanya kitu chochote kwa sababu vitu vinahitaji uelewa mpana wa source code zinazotumika kutengeneza application, mifumo pamoja na kuhakikisha usalama wa data (encryption).
Hakuna AI ambayo itaweza kumwondoa developer kwenye nafasi yake, bali itamsaidia asipoteze muda mwingi katika kutengeneza programu zake.
Mtaalamu wa Ethical hacking occupytheweb aliyeandika kitabu cha Linux Basics for Hackers anasema “AI is not perfect, yet not smarter than you. It’s not going to put you out of job if you’re studying a career in tech. You need to embrace AI as tool, use it like how you use google, or else you’re going to be left behind”.
Kama ushatumia AI katika coding zako utagundua kuwa, AI inatoa data kulingana na wewe unavyotaka.
Ubora wa uulizaji wako ndio ubora wa AI kukupa taarifa sahihi vinginevyo itakupa source code tofauti na unavyohitaji, hapo utakomaa na debugging mpaka basi, hata ukiirudishia ili idebug inakuzalishia error zingine kumi.
Wale wanaosema AI inaenda kuchukua nafasi za madeveloper wengi wao hawacode, ndio wapya kwenye game (beginners), wanaoona coding ni ngumu, tena hawa ndiyo wanaopiga makelele balaa.
Wale wanaofaidi matunda ya kucode ni wale wenye title kuanzia nne yaani ni (Front-end and Back-end Developer, Network Administrator, content writer, security expert etc).
Sio lazima ujue vyote kwa ufasaha, vingine ni vizuri ukawa na basic understanding ya ni kivipi zinatumika. Usikae na kitu kimoja tu jaribu kuwa two in one (department).
Saivi kuna AI zinazotengeneza website, Apps je, madevelopers tutakaa wapi?
Je kuna AI inayotengeneza mifumo?
Iko hivi, hiyo ndiyo kazi yako jifunze pia jinsi ya kuzitumia hizo AI na ukiwa kama developer jitahidi kujua vitu kwa undani zaidi, ili hata mtu akikupa kazi uifanye kwa weledi.
Watu wengi wako shallow. Kama unajua coding na unajua kutumia AI vizuri sisi siyo wenzako tena.
Lugha. Kuwa vizuri kwenye uandishi unaoshawishi, andika content ambazo zitamfanya mtu aseme au ajisemee huyu kijana au huyu binti anajua. Iwe kwenye website, application, software au branding.
Wengi wanafeli katika eneo hili, lugha ndio itakayokutofautisha kati yako na wengine ikiwemo AI.
Kuna siku utaajiriwa au utaitwa kufanya marekesho kwenye system ya kampuni fulani, sijui utamuuliza AI? Kumbuka AI ziko limited na hauwezi kuipa source code zote za system ya kampuni hiyo ili itambue tatizo ni nini. Ni wewe na uelewa wako.
Kama utaacha kucode, ukajiunga na kundi la watu wanaosifu na kupiga makelele kwamba AI inaenda kuchukua nafasi za developers. Ni kweli hao hao developers ndio watakaochukua nafasi yako.
Hakuna muda mzuri wa kukabiliana na unemployment kama muda ambao uko chuo.
Wengi huja kulifahamu hili tayari jua limeshazama, muda huo upo nyumbani, pengine hata kupata fedha ya kujikimu au ya vocha ni kipengele yaani kuipata ile buku mbili mpaka uende ukafanye kazi za vibarua ndio uipate.
Kitu kizuri ni kwamba leo hii upo chuo, unapokea boom, tukiongelea suala la bando kwako saivi siyo shida basi tumia muda huu kufanya mambo ambayo baada ya kumaliza chuo usihangaike kutafuta kazi.
Haya ndiyo mambo matano ambayo Mwanachuo unaweza kufanya ili kukwepa Unemployed baadae
1. Jiunge na mitandao ya kijamii muhimu kama vile Linkedin na Twitter
Linkedin au Twitter ndiko maarifa yalipo, huko utakutana na waajiri mbalimbali (Recruiters/Employers). Watu kama hawa inawezekana usiwaone kipindi unaanza ila jinsi utakavyozidi kuonyesha uwepo wako kwenye majukwaa hayo, ndivyo utakavyojiweka katika nafasi nzuri ya kupata fursa.
Huko utapata kujifunza mambo kadha wa kadha yanavyoenenda kwenye tasnia yako, pia itakusaidia kuelewa mapema ni nini ufanye ili baadae usije kupishana na gari la mshahara.
Itakusaidia kuelewa jinsi mambo yanavyofanyika kwenye industry unayosomea. Siyo unamaliza chuo, unaambiwa nafasi zipo na zinahitaji mtu anayejua vizuri Microsoft Access, ndiyo ukute na wewe ulivipuuzia kipindi upo chuo.
Katika ulimwengu tuliopo simu au laptop yako ni siraha tosha inayoweza kubadilisha historia ya maisha yako, itategemea tu unaitumia kwa namna gani. Jambo la kufanya install app ya Linkedin na Twitter sasa hivi.
2. Ongeza maarifa kupitia Online Courses
Internet imerahisisha maisha, leo hii unaweza kusoma popote ulipo na cheti ukitaka unapewa.
Course yoyote unayoitaka inapatikana mtandaoni ni suala la kuchukua simu na kuingia youtube, andika course unayotaka usome, mfano, Project Management full course, kwa click moja unamaliza course ukiwa na maarifa ya kutosha. Youtube inatoa course bure kabisa.
Pia kuna majukwaa mengi ambayo unaweza kuchukua course unayoitaka kama vile Linkedin learning, simplilearn, CompTIA+, Udemy, Coursera n.k huku unafundishwa real life experience tofauti na mwalimu darasani anaekufundisha ili amalize syllabus.
3. Kuwa vizuri kwenye lugha (written and spoken)
Asilimia 90% ya mazungumzo mtandaoni hufanyika kwa njia ya maandishi, hivyo ni vizuri ukajinoa zaidi katika kuandika na kuwasilisha maudhui/ujuzi wako kwa watu.
Njia nzuri ya kujinoa ni kuanza leo kwa kuandika mawazo uliyonayo kichwani kwenye notebook au applikesheni yoyote ikiwezekana uwe unapost hata kama kiingereza au kiswahili kimekaa upande. Practice makes more perfect.
Ukiwa chuoni jitahidi kupost kila siku au mara mbili kwa wiki kama vipindi vitakuwa vimebana, ule muda unamaliza chuo, utakuwa na kundi kubwa la watu wanaokuhitaji ufanye nao kazi au uwafanyie baadhi ya kazi zao.
Muhimu: Post vitu vya msingi ambavyo mtu akisoma aseme kweli huyu kijana au huyu dada anajua.
4. Anza kufanya kazi ukiwa bado upo chuo (freelancing au virtual internship)
Tafuta kazi ambazo unaweza kufanya ingali bado unasoma, huu ndio muda wa kujitolee kwenye taasisi, kampuni mbalimbali. Fanya kazi as a freelancer kwenye majukwaa mbalimbali kama vile Upwork, Freelancer, Fiverr, Remototask.
Muda mwingine vitu unavyofundishwa darasani nitofauti kabisa na vile vinavyofanyika kwenye industry, hivyo ni bora kuyajua haya mapema na kuyafanyia kazi ili pindi utakapomaliza chuo isiwe changamoto kwako.
Usisubiri mpaka umalize chuo ndio uanze kuomba kazi, najua unajua kule nyumbani hali ilivyo yaani kupata kazi ni mtiti, ukimaliza chuo ukaenda nyumbani, ndiyo imeisha hiyo.
5. Kuwa mtu mwenye haiba (personality) ili umma wa digitali uvutiwe na wewe
Kila siku jitahidi kuwa mtu wa tofauti na wengine, fanya vitu ambavyo watu wengi hawavifanyi ilimradi unaviamini, ni halali na hivyo utaonekana kuwa ni mtu wa pekee, na kwa upekee huo utajinyakulia fursa kedekede. Kuwa mtu wa kujifunza kila kukicha kwa kusoma vitabu, articles, hudhuria mikutano, seminar au online events.
Hakuna chuo kinachoweza kukufanya ukwepe unemployed baadae, zaidi ya kuweka juhudi zako binafsi katika kuitengeneza kesho yako. Hatima ya maisha yako ipo mikononi mwako.