Fahamu Mambo Matano Kuhusu Internship

Fahamu Mambo Matano Kuhusu Internship

Internship au tarajali imekuwa ni kimbilio kubwa la vijana wengi wanaohitimu chuo baada ya kukosa kazi.

Lakini ukweli kuhusu internship, vijana wengi wamekuwa wakiamini watapewa kazi moja kwa moja baada ya muda wa internship kuisha bila kujali upande wa pili. 

Hivyo wengi wanaishia kuendelea kupewa nafasi za kujitolea miaka hadi miaka. Kwa nini hawaajiriwi na ni nini hasa wanatakiwa kufanya?

Nimekusogezea mambo matano muhimu kuhusu internship.

Njia inayotumika kupata interns.

Mara nyingi nafasi za internship zinazotangazwa na makampuni hutumia njia zinazofanana sawa na zile zinazotumika kupata wafanyakazi wa kawaida japo interview zao zinatofautiana. Wote mtatuma maombi, mtaitwa kwenye interview na pengine kazi mtakazokuwa mnafanya zitakuwa ni sawa.  

Kwanini mtu wa intern/volunteer usilipwe hata pesa kidogo kiasi cha kuweza kumudu maisha yako ya kila siku? Wengi huenda kujitolea kwa lengo la kupata CV, uzoefu yaani ile dhana ya ili uajiriwe mpaka uwe na experience ya mwaka mmoja au zaidi. Wanasahau thamani yao katika kufanya hizo internship. 

Muda mwingine baadhi ya makampuni hayakupi pesa ya kujikimu kisa huna uzoefu wa kutosha, unajikaza kisabuni kwa imani ya kwamba siku moja utaajiriwa, kumbuka mambo yanabadilika inawezekana kazi uliyoisotea miaka ikaja kuchukuliwa na teknolojia. 

Zingatia haya maswali mawili ukiwa intern, lengo lako haswa la internship ni lipi ukiachilia mbali kuajiriwa kwenye hiyo kampuni?  Uhakika wa kupata kazi  baada ya internship upo au utaendelea kujitolea?

Ukiona kampuni haikuajiri ng’atuka wala usiendelee kujitolea labda kama wanakulipa pesa inayokidhi mahitaji yako kipindi unajitafuta. 

Muda uliowekwa kwa ajili ya internship

Internship ikidhidi miezi sita inaadha kupoteza ukweli wake yaani unaanza kuwa mfanya kazi wa bure au mwenye ujira mdogo. Makampuni mengine yanatumia mbinu hii kama fursa, utakuta mtu anajitolea miaka na miaka kisa zile pesa za kuitwa chimbo unapewa laki mbili maisha yanasonga. 

Ukweli kuhusu maisha haya wengi huumia ndani kwa ndani na kuona hakuna kazi zingine za kufanya, ndugu yangu kama upo kwenye hii hali chagua moja utafute maarifa mengine yatakayokuweka mjini au uendelee kung’ang’ana na internship ambazo hufurahishwi nazo.

Dhana ya Waajiri wengi nchini

Baadhi ya taasisi na makampuni mengi nchini yamegundua internship ni njia rahisi ya kupata wafanyakazi wengi hasa wahitimu vyuo “hapa tukimweka intern si itakuwa poa”.

Ni kweli kwamba wanaohitimu mavyuoni wengi wao hawana uzoefu wa kutosha kwenye hizo kazi. Inakuwaje mtu amefanya internship halafu asiajiriwe (nidhamu mbovu au)

Maofisini kuna changamoto zake, kwa unayetamani kufanya kazi kwenye makampuni ya aina hii hauna budi kuwa na nidhamu ya hali ya juu, ujitume ili uonekane la sivyo waajiri hawana msaada na wewe.

Internship ni kwa ajili ya wanafunzi

Kwa kawaida internship inabidi ziwahusu sana wanafunzi walioko elimu ya kati na juu. Na hili jukumu si la kutegemea sana serikali, Mwanafunzi mwenyewe yampasa atafute kampuni au taasisi kwa ajili ya kujitolea (internship) kadri iwezekanavyo kabla hajahitimu. Anaweza kufanya kazi either kwa kuhudhulia mguu kwa mguu kwenye hiyo taasisi au kupitia mtandao (virtual internship).

Hii itamsaidia kupata uzoefu wa kazi ili kipindi atakapomaliza masomo asianze kuhangaika kutafuta nafasi za kujitolea bali kutafuta kazi. 

Sanjali na hilo kuna kujiajiri, hapa nazungumzia uwezo wa kufanya kazi zako binafsi kwa kutumia uzoefu ulioupata mfano kuanzisha internet cafe, kufungua biashara, kusimamia mitandao ya kijamii ya kampuni husika au kutengeneza mifumo kwa watu wa coding(programming).

Je Unatakiwa kufanya nini?

Kuna njia mbili za kufanya kwa kijana unayetazamia kuiona kesho yako yenye mafanikio.

 1. Fanya internship ambayo utakuwa unalipwa angalau kiasi fulani cha pesa huku ukiweka malengo yako sawa, usiwe mtu wa internship kila siku na ikitokea,kupata kazi kwenye makampuni imekuwa ni changamoto fikiri point ya pili.
 1. Mjenzi wa maisha yako ni wewe mwenyewe, umetafuta kazi kwenye makampuni, taasisi na umekosa. Ni muda sasa wa kukaa na kutafakari kazi binafsi zitakazokuingizia kipato, unaweza kujaribu mtandaoni  kazi za freelancing.

Hayo ndiyo mambo muhimu ya kuzingatia katika safari yako ya kuitengeneza kesho.

Ukweli Kuhusu Kupata Wateja Mtandaoni (Darasa Muhimu)

Ukweli Kuhusu Kupata Wateja Mtandaoni (Darasa Muhimu)

Watu wengi wanalalamika biashara zao hazipati wateja mtandaoni pamoja na kwamba wanapost bidhaa zao Instagram, WhatsApp na kwenye majukwaa mengine ya digitali.

Wengine huanza kufikiri pengine kufungua website itasaidia kupata wateja kuliko kuwa na Instagram au WhatsApp pekee.

Wengine hudhani kununua akaunti yenye followers wengi basi itasaidia kupata wateja. Wanatafuta akaunti inayouzwa, yenye followers 10K au zaidi, wananunua. Lakini bado hawapati wateja. Na hata kile wanachokipost hakipati likes wala comments pamoja na kuwa na followers wote hao.

Hata matangazo ya kulipia (sponsored ads) hayawasaidii. Wanajikuta wanapoteza pesa tu.

Wengine wanawalipa “wataalamu” wa social media wanaojitangaza wanakuza akaunti na kuongeza followers. Followers kweli wanapata, lakini kuuza bado inabaki changamoto!

Hayo yote niliyoyataja hapo juu ni baadhi ya malalamiko tunayopata kila wiki kutoka kwa wajasiriamali wanaouza bidhaa mtandaoni. 

Malalamiko haya pamoja na maswali mengine tunayapata kupitia kampuni yetu,Tanzlite Digital, inayosaidia wafanyabiashara kukuza biashara zao na kujipatia wateja kupitia majukwaa ya digitali.

Malalamiko ni mengi. Nitatumia  makala hii kueleza ukweli kuhusu kupata wateja mtandaoni.

Nini Kinafanya  Watu Wanunue Bidhaa yako Mtandaoni?

Zipo sababu kuu tatu zitakazokufanya uuze bidhaa mtandaoni: 

 1. Soko na Bidhaa yenyewe.
 2. Jina lako mtandaoni (Watu wanakufahamu?)
 3. Uwezo wako kushawishi kupitia Maudhui.

Ubora na Soko la Bidhaa Yako

Hapa naomba tuelewane. Kama kitu unachokiuza ni kile ambacho watu wanaweza kukipata kwa urahisi mtaani kwao —basi hutopata wateja mtandaoni. 

Kwanini wanunue kwako wakati bidhaa hiyo hiyo inapatikana kwa mangi au na maduka mengine ya karibu?

Jiulize; unaweza kuuza soda mtandaoni? Au wembe au majani ya chai? 

Kama kila mtu anauza kile unachotaka kukiuza mtandaoni basi inabidi uwe na OFA nzuri, au kuwe na ubunifu na namna ya uwasilishaji bidhaa yako kwa watu ili kujitofautisha na wengine. Vilevile ujenge mahusiano mazuri na wateja wako ili waendelee kurudi na kuwaambia wengine.

Lakini kwa bidhaa kama vile karanga, mchele, vitenge, na baadhi ya nguo  —hizi zinapatikana kila mahali. Usishangae kuona hupati wateja mtandaoni. 

Watu hawatafuti mtandaoni vitu ambavyo vinapatikana kila kona mtaani kwao. 

Ili kupata wateja mtandaoni, bidhaa yako inatakiwa kuwa na upekee, ubora na soko lake liwe halijachuja (saturated) kwa kuwepo wa utitiri wa bidhaa hiyo kila mahali. Tofauti na hapo, ni bora ufungue duka mahali penye mzunguko mkubwa wa watu (foot traffic). Kama vile Kariakoo.

Mitandao inasaidia kufikisha bidhaa yako kwa watu wengi. Lakini kuuza inategemea na bidhaa yenyewe.

Jina Lako Mtandaoni (Brand Authority)

Kule Instagram wapo watu wanauza bidhaa za aina mbalimbali kama vile nguo, viatu, na electronics. Lakini yapo majina machache maarufu kama vile (kwa Tanzania) Vunja Bei, Frank Knows, David Sportwear, na kadhalika.

Hao na wengine wengi wenye waliojitengenezea jina mtandaoni wanapata wateja na kuuza bidhaa zao.

Unajua kwanini wanauza? Ni kwa sababu watu hupenda kununua kitu kutoka kwa mtu wanayemfahamu, au wamewahi kumsikia, au watu wengine wanamuongelea.

Je wewe umetengeneza jina? Hakuna mtu yuko tayari kukutumia pesa ikiwa hakufahamu, hajawahi kukusikia, wala haoni watu wengine wakikuongelea. Hapa watu kukuongelea maana yake angalau kuwe na comments kwenye post zako mtandaoni.

Naomba nitoe mfano. Kuna watu wanauza bidhaa za makampuni ya network marketing au MLM kama vile BF Suma na Forever Living.

Hawa watu wanashida kubwa. Kwanza kabisa wamepigwa pesa yao ambayo hawataweza kuirejesha kuuza bidhaa hizo. Pili wewe siyo daktari, siyo mtaalamu wa lishe, huna pharmacy, na huna zahanati. Isitoshe huna hata mtu mmoja uliyemponya kwa dawa zako. Dawa yenyewe unasema inatibu “magonjwa mbalimbali”. Kwa kifupi hauna authority ya kumshawishi mtu anunue bidhaa kutoka kwako.

Tatizo siyo bidhaa, tatizo ni nani anauza hiyo bidhaa.

Narudia tena; watu hawanunui bidhaa bali wananunua jina la mtu linalohusiana na bidhaa hiyo. Daktari akikuandikia dawa, unaenda kuinunua na kumeza si kwa sababu unaijua hiyo dawa (inaweza isiwe bora) bali kwa sababu unamwamini daktari.

Nikupe mfano mwingine, hivi majuzi tajiri Elon Musk alitangaza bidhaa mpya ya pefume. Ndani ya masaa machache aliweza kuuza chupa 10,000 kwa bei ya dola za kimarekani 100 kila chupa. Jamaa alitengeneza dola milioni moja ndani ya masaa tu.

Hiyo ndiyo nguvu ya kuwa na jina. Tengeneza jina kwanza halafu kuuza mtandaoni itakuwa rahisi. 

Kutengeneza jina mtandaoni si kuwa maarufu (fame, celebrity). Ni kujenga taswira yenye kuaminika miongoni mwa watu unaowalenga. 

Kumbuka, Kuwa na Jina Mtandaoni Siyo Umaarufu. 

Hapo awali nimesema ili uuze mtandaoni lazima uwe na jina. Hapa simaanishi umaarufu (fame, celebrity). Hapana. Jambo la msingi ni kuhakikisha unatengeneza jina miongoni mwa watu unaowalenga kununua bidhaa yako. Si lazima Watanzania wote wakujue. 

Kama watu 1000 wamekufollow baada ya kuona unachouza basi hilo ndilo jeshi lako. Kama wamekufollow kwa hiari maana yake wamevutiwa na unachokifanya. Endelea kuwapa maudhui bora (waelimishe, wachekeshe, wape mbinu za kutumia bidhaa yako n.k). Hao watu 1000 wanaweza kusambaza habari zako kwa wengine na hivyo ndivyo utakua na kujipatia jina. 

Lengo ni kujiweka katika mazingira mazuri ya kuvutia wateja. Hakikisha profile inavutia, haina makosa au picha zisizo na ubora.

Hapa pia naomba nikazie jambo; kununua followers ni kupoteza pesa zako. Epuka mtu anayekwambia atakupatia followers. 

Uwezo wa Kushawishi Wateja 

Unaweza kuwa na bidhaa nzuri lakini ukashindwa kushawishi wanunuzi. Unaweza kuwa na dawa inayotibu kansa lakini watu wasiamini kwa sababu huna ushawishi. 

Hii ni changamoto ya kushindwa kufahamu saikolojia ya mteja unayemlenga pamoja na kushindwa kuandaa maudhui (content) yenye mvuto na yenye kushawishi. 

Jiulize; zile picha, video na maandishi unayopost mtandaoni yana nguvu ya kushawishi? Yana mvuto? Picha ni kali au ni low quality?

Yote hayo yanachangia kama watu watavutiwa na kukuamini au hawatavutiwa na kukutilia mashaka.

Kwa mfano tuseme unauza pazia. Badala ya kusema; OFA! Jipatie Mapazia Mazuri kwa Bei Nafuu. Tunapatikana Kariakoo

Unaweza kusema; Pendezesha Nyumba Yako kwa Pazia Nzuri Ili Wageni Wakija Waone Kweli Wapo Ndani Ya Nyumba

Wanawake hawanunui pazia bali wananunua UFAHARI wa kupendezesha nyumba. Wakienda kununua pazia swali wanalojiuliza kichwani ni “Pazia gani litapendeza ndani ya nyumba yangu?”. 

Jaribu kucheza na saikolojia ya mteja unapoandaa maudhui ya kupost Instagram au popote unapopatia wateja. Onyesha Matokeo; nini mteja atapata akinunua bidhaa yako? Je atapata mwonekano mzuri? Je chumba chake kitapendeza? 

Katika kuandaa maudhui, onyesha matokeo ya bidhaa. Usionyeshe bidhaa.

Badala ya kupiga picha mabaro ya vitenge dukani kwako, piga picha ya mwanamke aliyevaa kitenge na kupendekeza. 

Badala ya kupiga picha mapazia uliyotundika dukani mwako, piga picha pazia zilizotundikwa ndani ya nyumba. Watu hujaribu kutengeza picha kichwani ya namna gani nguo itaonekana wakiivaa, au pazia litaonekanaje likiwa ndani ya nyumba. Usionyeshe tu bidhaa, onyesha matokeo. 

Ukiwafahamu wateja wako vizuri, na bidhaa yako ikawa iko vizuri, basi hata yale matangazo ya kulipia yatazaa matunda. Vinginevyo utakuwa unachoma pesa.

Hitimisho: Ukweli Kuhusu Kupata Wateja Mtandaoni 

Mitandao ni njia tu ya wewe kufikisha bidhaa yako kwa walengwa. Kuhusu kuuza au kutokuuza inatokana na sababu nyingi ikiwemo bidhaa yenyewe, soko, pamoja na uwezo wako wa kushawishi. 

Kwa ujumla mitandao imerahisisha sana jinsi ya kufikia wanunuzi wa bidhaa za watu. Bila mitandao kama WhatsApp, Instagram, YouTube, Tovuti na mingineyo, watu walio mbali wasingeweza kuona bodhaa yako na kuwasiliana nawewe. 

Kila mtu anaweza kuuza chochote mtandaoni mathalani kitu hicho kina soko na muuzaji anaweza ku-supply hiyo bidhaa.

____________

Asante kwa kusoma makala hii. Naitwa Shukuru Amos, ni mwandishi na mtaalamu wa masoko ya digitali (Digital Marketing). Wasiliana nami kwa WhatsApp hapa

Share makala hii kwa mfanyabiashara mwingine.

Fahamu Fursa Nne Zinazopatikana Kidigitali

Fahamu Fursa Nne Zinazopatikana Kidigitali

Mara nyingi umekuwa ukisikia watu wanaongelea kuhusu fursa unazoweza kufanya kupitia majukwaa ya kidigitali lakini bado hujajua hizo fursa ni zipi, na unawezaje kuzipata? Kwenye makala hii nitakuelezea kwa ukaribu hizo fursa, namna ya kuzipata na jinsi ya kuzitumia ili kujiingizia kipato.

Majukwaa ya kidigitali yamekufungulia dunia kuwa unachotaka, fursa zote unazo kiganjani mwako. Unaweza kufanya biashara yako binafsi kupitia hii hii mitandao na kujipatia kipato au kufanya kazi na mtu yeyote kutoka sehemu mbalimbali bila kuonana uso kwa uso. 

Kitu chochote unachoweza kufanya kidigitali na kikakuletea faida hiyo ni fursa.

Mfano, Natoa huduma za kupamba kumbi za sherehe, nitaanza kushare picha zikinionyesha napamba kumbi mbalimbali kwa ajili ya sherehe tofauti kama harusi, mikutano, sendoff au kitchen party ili atakayeona na kuvutiwa anitafute tufanye kazi. 

Hivyo ndio jinsi fursa za kidijitali zilivyo kuuza ujuzi au bidhaa zako mtandaoni kwa watu wengi kwa mara moja. Kuna Aina nyingi za Fursa mtandaoni ni wewe tu kuchagua ipi itakufaa

1.      Kuuza Huduma zako(Services)

Hii inaweza kuwa huduma unayoitoa wewe mwenyewe binafsi au kama kampuni. Mfano kufundisha au kusherehesha. Dukahuru anapatikana Instagram akifundisha watu wengine jinsi ya kuuza bidhaa mtandaoni na huduma nyingine nyingi. 

Kama wewe unaweza kufanya hivyo basi hiyo ni fursa ikimbilie mapema.

Huduma ya kikampuni ni kama ile anayofanya Haika Lawere anakodisha kumbi zake kwaajili ya sherehe, vikao au makongamano. Pale instagram huwa anapost picha za kumbi, bei na mawasiliano kwa atakayehitaji.

Wewe kijana au wewe ndugu yangu uliye kwenye kampuni na una matazamio ya kupata chochote kutokana na hilo kampuni unalofanyia kazi, tumia muda huo kuji-promote kwa kutumia status ya kampuni ili hata siku umetoka, utoke na jina.

Kwa yule mwenye uwezo wa kufanya kama Haika basi fanya, hiyo pia ni fursa itakayofanya usihangaike kutafuta fursa zingine. 

2.      Kuuza bidhaa zako binafsi (Products)

Mfano; unamiliki duka la kuuza mafuta ya nywele, una simu janja, jiunge mtandao wa Instagram, fungua kurasa yako na anza kupost mafuta yako unayouza, kumbuka jinsi utakavyojinadi katika bidhaa yako ndivyo utakavyoweza kupata wateja. 

Hapa nazungumzia jinsi ya kupost(maudhui). Watu mbalimbali wataona bidhaa yako na watakutafuta ili hali uliweka mawasiliano kwenye kurasa yako.

Je, ushawahi kununua kitu mtandaoni? Kama jibu ni ndiyo basi hata wewe unaweza kuuza kitu chochote mtandaoni. Unahitaji tu kujua wateja wako wanapatikana mtandao upi, jifunze jinsi ya kutumia mtandao husika vizuri na upeleke biashara yako huko.

3.      Kuuza bidhaa za watu wengine (Affiliate Marketing)

 Kama hauna mtaji wa kuanzishia biashara yako na hauna biashara yoyote unayoifanya. Tafuta kampuni au biashara ya mtu ambaye utakuwa unamsaidia kutafuta wateja mtandaoni au kufanya biashara yake ijulikane kwa watu wengi. 

Mtu anayefanya kazi ya affiliate marketing hulipwa kutokana na mauzo yatokanayo na juhudi zake za kuleta wateja. Hii unaweza kuifanya kwenye blog, tovuti yako binafsi au kwenye mitandao ya kijamii. 

Pia kuna makampuni yana bidhaa zao na yanatafuta watu wa kuwasaidia kuuza au kuwafikia wateja na kwa kila mteja utakayemleta utapewa Kamisheni.

Kamisheni ndo itakua faida yake kutokana na makubaliano mtakayoweka. 

4.      Kushawishi watu kununua bidhaa Fulani (Influencing)

Hii inatumiwa sana na makampuni mbalimbali makubwa na madogo. Kutafuta watu wenye ushawishi mtandaoni kuweza kushawishi watu watumie huduma au bidhaa zao. Na utalipwa kwa makubaliano mtakayoweka. Mfano Lilian Lema anafanya hii kazi Instagram na kulipwa.

Utahitaji kuwa na page yako ambayo umeijenga mwenyewe na kupata wafuasi ambao utaweza kuwashawishi. Sio lazima uanze ushawishi kwa kulipwa unaweza fanya bure na badae ukaanza kuchaji watu wakitaka huduma hiyo kwako.

Hili ndo somo langu la leo kuhusu fursa za kidigitali, haimaanishi ndio mwisho wa fursa, Hapana. Kutokana na hizo nne unaweza pata fursa nyingine zaidi. Muhimu ni kujiamini unaweza na kuanza kufanya.

Jinsi ya Kutengeneza M-Pesa Visa Card Nchini Tanzania

Jinsi ya Kutengeneza M-Pesa Visa Card Nchini Tanzania

Hauhitaji tena Kwenda Bank kufungua akaunti ili upate kadi itakayokuwezesha kufanya malipo mtandaoni, hapa kikubwa una akaunti ya M-Pesa. Au unataka usitumie kadi yako ya CRDB/NMB kufanyia malipo mtandaoni?

Chukua simu yako, fuatilia makala hii itakayokusadia kufahamu jinsi ya kutengeneza Mpesa VISA card hatua kwa hatua na uzuri wake hakuna gharama yoyote utakayotozwa na haichukui zaidi ya dakika moja tayari unakuwa na kadi yako.

Kabla hatujaendelea tufahamu kwanza Mpesa visa kadi ni nini kwa undani wake.

M-Pesa Visa kadi ni nini?

Hii ni kadi mbadala ambayo humwezesha mtu kufanya malipo mtandaoni pindi anapokuwa ananunua bidhaa au huduma yoyote mtandaoni.

Kadi hii inaruhusu kutumia pesa zako zilizopo kwenye akaunti ya M-Pesa kufanya malipo yoyote ya kidigitali bila kuhamisha pesa Kwenda kwenye akaunti yako ya Bank.

M-Pesa Visa Kadi siyo kadi ya mkopo bali ni kadi ya malipo inayotengenezwa kupitia njia ya Mpesa tu yaani STK, USSD au App.

Baada ya kutengeneza M-Pesa Visa Kadi utapokea ujumbe wenye taaarifa zote kuhusu kadi yako ikiwemo kadi namba, tarehe itakayo-expire, CVV (Card Verification Value) namba.

Ili uweze kufanya malipo mtandaoni ni lazima uweke pesa kwenye kadi hiyo mara tu baada ya kuitengeneza au pale unapotaka kununua kitu.

CVV ni nini?

Baada ya kutengeneza kadi utatumiwa CVV namba, je CVV ni nini? Ni namba za usalama ambazo huwasaidia wamiliki wa tovuti kuhakiki kama kweli wewe ni mmiliki halali wa hiyo kadi, pia husadia kupunguza udanganyifu unaoweza kufanyika kutoka kwenye kadi yako ya M-Pesa.

Bila CVV namba huwezi kufanya muamala wowote ule. Namba hii pia inasimama kama nywila ya kadi yako unapotaka kununua kitu mtandaoni.

CVV zinafanya kazi ndani ya dakika 30 za mwanzo baada ya malipo kufanyika na hii husaidia kadi yako isitumiwe na mtu mwingine ambaye kwa bahati mbaya anaweza kujua taarifa za kadi yako na pia asiweze kubadilisha CVV namba. Hizo CVV zikishabadilishwa basi huwezi tena kuitumia hiyo kadi yako. Kuwa nazo makini.

Jinsi ya Kutengeneza M-Pesa Visa Kadi Nchini Tanzania.

Fuata hizi hatua kufanikisha zoezi hili,

 1. Bofya *150*00#.
 2. Chagua namba 4 LIPA kwa M-PESA.
 3. Chagua namba 6 M-Pesa VISA Card.
 4. Chagua namba 1 Tengeneza Kadi.
 5. Baada ya kufanikisha kutengeneza kadi, utapokea ujumbe wenye taarifa kuhusu kadi yako.

Jinsi ya Kuangalia Huduma Mbalimbali Kwenye Kadi Yako

 1. Bofya *150*00#.
 2. Chagua namba 4 LIPA kwa M-PESA.
 3. Chagua namba 6 M-Pesa VISA Card.
 4. Baada kuchagua namba sita utaona list ifuatayo (Tengeneza kadi. Taarifa za kadi. Weka Pesa kwenye Kadi. Salio la Kadi. Kadi Yangu. Msaada.)

 Kwenye M-Pesa App

 1. Fungua M-PESA APP.
 2. Chagua Services tab.
 3. Chagua M-PESA Visa Card.
 4. Bofya Tengeneza M-PESA Visa Card.
 5. Baada ya hapo utapokea ujumbe wenye taarifa zako za kadi.

Utofauti wa Mpesa Visa card na MasterCard

Utofauti wake ni kwamba Mpesa Visa card inatumika kufanyia malipo mtandaoni tu, mwenye uwezo wa kuweka pesa (top up) kwenye hii card ni mmiliki pekee, huwezi kutumia kadi hii kwa lengo la kutumiwa pesa kutoka upande wa pili ikiwa MasterCard inaweza kutuma na kutumiwa pesa, kufanya malipo mtandaoni na mwisho kabisa card hii ni lazima iwe inashikika.

Mpesa visa card ni kwaajili ya malipo tu.

Huduma hii ya M-Pesa na Visa nchini Tanzania inaondoa kabisa haja ya kuwa na akaunti ya CRDB/NMB ili kufanya malipo mtandaoni kitaifa na kimataifa.

Kwa usalama zaidi, inashauriwa kurekodi maelezo ya kadi yako mahali salama na kufuta ujumbe wa nakala za Visa Kadi ya Mpesa kutoka kwenye Simu yako! ili kujiepusha kuvuja kwa taarifa zako za kadi.

Vodacom wamerahisisha maisha kwa kuweka uhusiano huu unaowawezesha watumiaji wa M-Pesa kufanya malipo kidigitali kupitia mtandao wa Visa wenye zaidi ya wafanyabiashara milioni 100.

Hivyo ndivyo unaweza kutengeneza M-Pesa Visa Card kwa ajili ya kufanya malipo yoyote mtandaoni.

Ahsante kwa kusoma Makala hii naitwa Anthony charles.

Njia Bora Ya Kujenga na kukuza Jina Mtandaoni

Njia Bora Ya Kujenga na kukuza Jina Mtandaoni

Haijalishi kuwa wewe ni mtoto wa mkulima, huna connection, umetafuta kazi umekosa, watu hawakujui au upo kwenye harakati za kujitafuta. Chukua simu yako zama mtandaoni huko ndiko fursa zilipo.

The universal does not belong to anyone group of people, everyone story is potentially universal it just need to be told well by Chimamanda Adichie

Tupo kwenye ulimwengu wa kidigitali ambao kila mmoja wetu anatumia mitandao ya kijamii kama Linkedin, Twitter, Instagram na Facebook ambapo kuna uwezekano mkubwa wa kujipenyeza nakujenga jina katika majukwaa hayo.

Imebaki kwako, kama Joti anajulikana kwa kuchekesha, wewe utajulikana katika lipi?

Kuna umuhimu gani wa kujenga jina mtandaoni?

Swali zuri, haujengi jina peke yake bali unajitengenezea mazingira mazuri ya kuondokana na kile wanachokiita unemployment na kuwa kwenye uwanja mzuri wa wajasiriamali.

Uwanja ambao hata kama baadae ukija kuanzisha biashara yako iwe ni rahisi kuaminiwa na kupata wateja kwa urahisi. 

Kutengeneza jina mtandaoni ni sawa na kuwa na bima ambayo itakusaidia wewe usihangaikei pindi mambo yatakapoenda ndivyo sivyo.

Saivi ni kawaida mtu kumaliza chuo na kurudi nyumbani kwenda kulima viazi, mwajiriwa kuendelea kutegemea mshahara, kuendelea kujitolea kwa sababu hakuna namna nyingine itakayomfanya apate pesa. 

Ulishawahi kusikia watu wanafanya kazi kama freelancer, yaani mtu aliyeko Washington Dc anampa kazi mtu aliyeko Tanzania? Huko ndiko kuzisaka fursa mtandaoni.

Unaikumbuka hii sauti “Tunakufungulia dunia kuwa unachotaka” au “Dunia ipo kiganjani mwako”

Ni njia zipi zitakazokusaidia kujenga na kukuza jina mtandaoni?

Unataka kuwa nani?

Hata nchi yenyewe huwa inaweka malengo ya muda mrefu na ya muda mfupi. Pasipo malengo ni sawa na kuendesha gari huku umesinzia. 

Kama tayari unajua baada ya miaka mitano unataka kuwa mtu fulani ni vizuri zaidi na kama bado hujajua chukua kalamu yako, andika malengo yako pembeni, njia hizo zisipo fanya kazi basi jitafute mpaka ujipate. Mali bila daftari huisha bila kujua. 

Je kweli umeandika? Hii itakusaidia pale unapoanza kukuza jina lako mtandaoni kwa kuangalia zaidi malengo yako yanasemaje, isije ikawa unatwanga maji kwenye kinu.

Unataka ujulikane katika lipi?

Watu wakianza kusema napenda unavyoongea, napenda idea zako n.k maana yake umeweza kujitofautisha na wengine.

Ukisikia diamond, Patrick lumumba amearikwa kwenye tamasha, unafikiri ni nini kitaenda kufanyika? Vipi ukisikia Elon Musk, Steve Job au putin?.

Hivyo ndivyo inabidi ujulikane katika mitandao, inakuwa ni rahisi watu kukujua na kukufuatilia. Mtu akiona tu profile yako anajua huyu ni fulani anazungumzia vitu fulani, simple like that.

NB: Hapa kidogo inahitaji juhudi na uvumilivu kwa sababu mwanzoni utahangaika sana, hakuna likes, hakuna comment yoyote, hakuna mtu anayeonekana kukusupport lakini kumbuka malengo yako yanasemaje na endelea kusonga mbele. Kitu kizuri lazima ukihangaikie. Ukweli ni kwamba watu wanaona na kusoma post zako kila siku.

Ni mitandao ipi uwepo?

Kulingana na malengo yako chagua majukwaa yasiyozidi matatu ili uwe na uwezo wa kuyahimili mfano Linkedin, Youtube, Twitter, Instagram. 

Kukuza jina katika majukwaa haya kama nilivyo sema ni shughuli kidogo inakubidi ujitume kuwa active, onyeshe uhai wako kwa kupost, kushiriki kwenye post za watu wengine. Jinsi watu wanavyoona profile yako kila siku ndivyo wanavyozidi kukumbuka.

Ni maudhui gani upost?

Post chochote kama profile yako inavyojieleza hakikisha post zako ziwe kwenye mazungumzo yaani mtu akiwa anasoma awe kama vile anaongea na wewe tofauti na hapo post zako zitaonekana zimeandikwa na Chatgpt, hazina mguso. 

Hakikisha unatumia style mbali mbali katika kuwasilisha maudhui yako ili usiwachoshe wasomaji mfano tumia image, graphics, texts au short video kama ni itakupendeza.

Kitu kinachokufanya uonekane tofauti na wengine ni historia yako pamoja na vitu unavyovifanya katika hadhara ya mamilioni ya watu, wataalamu wa sales and marketing wanasema ujiuze.

Social media is indeed the best way to build an audience as it’s reach is global and connecting is as easy as  few clicks ~ Jules Marcoux

Post yako lazima iwe

 • Inalenga mtu au kundi fulani la watu
 • Inatatua changamoto fulani
 • Inaelimisha jambo fulani na 
 • Siyo, from no where umekula zako sangala unaenda kujipost. 

Fahamu hadhira yako.

Watu wote mtandaoni hawawezi kuwa hadhira yako, ni lazima uchague aina fulani ya watu ambao ndiyo target yako. Mtandaoni kuna watu wa kila aina, siyo lazima kila mtu akujue okay! au wewe umewahi kwenda kununua nguo buchani?

Kujenga jina maana yake ni kujenga mahusiano mazuri na watu unaowalenga, watakao furahia uwepo wako na walioko tayari kupokea kile utakachowapatia. 

Watu hununua bidhaa au maarifa kutoka kwa watu wanaowajua na kuwaamini. Soko ni watu na watu wako mtandaoni, wafuate huko huko waliko.

Ni matumaini yangu umejifunza kitu. Ahsante ndugu.


Naitwa Anthony Charles, Mwandishi katika blogu za Tanzlite

Fahamu Namna Nzuri Ya Kutumia Mitandao Ya Kijamii?

Fahamu Namna Nzuri Ya Kutumia Mitandao Ya Kijamii?

Je, mitandao inakutumia zaidi kuliko unavyotakiwa kuitumia?. Leo hii mtu akinunua simu kubwa (smartphone) kitu cha kwanza anachokimbilia ni kujipost mtandaoni hata kama yuko kitandani, je hivi ndivyo tunavyotakiwa tuitumie mitandao?

Kuwa kwenye ulimwengu wa kidigitali kunafanya watu wengi washindwe kuzikabili hisia zao. Pia wengi hawana uelewa kuhusu namna nzuri ya kuitumia mitandao hii.

Unajipost kila siku mtandaoni, unaeleza hisia zako kuhusu wewe, angali bado kijana ambaye hujui hata kesho yako itakuwaje. Picha isiyo na maadili ukishaipost mtandaoni hiyo imeenda, watu wataiona  na itahifadhiwa kwenye algorithms.

Basi, hata kama unajipost hakikisha hiyo picha inatunza heshima yako na inaleta mantiki kwa mtu yeyote. Muda huo angalau jifunze skills zitakazokusaidia kutengeneza ajira yako mwenyewe.

Mfano, Tuseme kampuni fulani inataka ikuajiri je, ikiangalia picha zako mtandaoni utafaa kweli kupewa hiyo kazi? Kwa sababu jinsi unavyojipost ndivyo unavyojielezea zaidi kuwa wewe ni nani, ni wa aina gani, unafanya nini, unapenda nini, uko makini kiasi gani?

Picha zako mtandaoni ni ushahidi tosha watu kukujua vizuri kuliko unavyojijua.

Mitandao ni sehemu ambayo unaweza kutafuta kupata fursa, kujifunza maarifa mbali mbali kutoka kwa watu wengine.

Itumie mitandao katika miradi hiyo na si kuvimbiana au kujionyesha kana kwamba upo kwenye maonyesho.

Ndiyo maana ni ngumu sana vijana kutoboa kupitia mitandao ya kijamii. Ukiangalia wanigeria au wakenya wanakimbiza soko kimataifa kupitia hii hii mitandao. 

Ziko wapi ajira? Ni sauti ya kila kijana baada ya kuhitimu chuo. Mitandao ni fursa shituka, tangaza kitu kinacholeta mantiki kwa watu usitangaze hisia zako.

Unaweka nini kwenye akili za watu pale wanapoona ulichokipost? Ifikie mahari uwe na fikra za mbali baada ya miaka mitano mbele, kile ulichokipost kitakutambulisha kama nani? 

Tunaishi kwenye ulimwengu wa kidigitali ambao mtu anaweza kufanya kazi remotely, itafika muda baadhi ya ajira kama siyo zote zitakuwa zinatolewa baada ya waajiri kukuona mtandaoni unafanya kitu fulani ambacho wanauhitaji nacho.

Soko la kimataifa linahitaji watu wanaoweza kufanya kazi kama freelancer (mtendaji huria).

Na atakayepata bahati hii ni yule ambae account zake za mitandao ya kijamii inajieleza yenyewe vizuri kuhusu yeye, na yuko active. Hakuna kutuma maombi wala interview labda iwe ni lazima. Mtu huyu atashuhudia message ikiingia au akipigiwa simu zikisemaHabari,

Nimekuona kwenye mitandaoni ukielezea zaidi kuhusu blablaa ah! nimekuwa nikikufuatilia toka muda …, vipi unaweza kunisaidia kufanya hili jambo fulani?

Noah Harari Alisema “We are going to believe more on algorithms than we believe in ourselves”.

Japo watu wengi hawajui ni kwa namna gani google hacking inaweza kutumika kupata taarifa zako nyeti binafsi, ni kwa namna gani active attack inaweza kufanyika kwa mtu binafsi au kwenye taasisi?. Na kibaya zaidi watu wengi hawaamini haya mambo utasikia, hii technolojia bado sana kwetu, nani atani-hack mimi wakati hata pesa sina? Ni sawa lakini haya pia yanaweza kutokea.

Tabia ya kupost maisha yako au familia yako kwenye mitandao siyo nzuri na inaweza kukugharimu baadae.

Si kuna watu wanasoma cybersecurity nchi hii, subiri baada ya miaka mitano tutakuwa na vijana wengi ambao hawana ajira na kazi yao itakuwa ndiyo hiyo KUHACK.

Tumia mitandao ya kijamii katika namna ambayo haitakuja kuharibu heshima yako. Ahsante ndugu.