Ukweli Kuhusu Kupata Wateja Mtandaoni (Darasa Muhimu)

Ukweli Kuhusu Kupata Wateja Mtandaoni (Darasa Muhimu)

Watu wengi wanalalamika biashara zao hazipati wateja mtandaoni pamoja na kwamba wanapost bidhaa zao Instagram, WhatsApp na kwenye majukwaa mengine ya digitali.

Wengine huanza kufikiri pengine kufungua website itasaidia kupata wateja kuliko kuwa na Instagram au WhatsApp pekee.

Wengine hudhani kununua akaunti yenye followers wengi basi itasaidia kupata wateja. Wanatafuta akaunti inayouzwa, yenye followers 10K au zaidi, wananunua. Lakini bado hawapati wateja. Na hata kile wanachokipost hakipati likes wala comments pamoja na kuwa na followers wote hao.

Hata matangazo ya kulipia (sponsored ads) hayawasaidii. Wanajikuta wanapoteza pesa tu.

Wengine wanawalipa “wataalamu” wa social media wanaojitangaza wanakuza akaunti na kuongeza followers. Followers kweli wanapata, lakini kuuza bado inabaki changamoto!

Hayo yote niliyoyataja hapo juu ni baadhi ya malalamiko tunayopata kila wiki kutoka kwa wajasiriamali wanaouza bidhaa mtandaoni. 

Malalamiko haya pamoja na maswali mengine tunayapata kupitia kampuni yetu,Tanzlite Digital, inayosaidia wafanyabiashara kukuza biashara zao na kujipatia wateja kupitia majukwaa ya digitali.

Malalamiko ni mengi. Nitatumia  makala hii kueleza ukweli kuhusu kupata wateja mtandaoni.

Nini Kinafanya  Watu Wanunue Bidhaa yako Mtandaoni?

Zipo sababu kuu tatu zitakazokufanya uuze bidhaa mtandaoni: 

  1. Soko na Bidhaa yenyewe.
  2. Jina lako mtandaoni (Watu wanakufahamu?)
  3. Uwezo wako kushawishi kupitia Maudhui.

Ubora na Soko la Bidhaa Yako

Hapa naomba tuelewane. Kama kitu unachokiuza ni kile ambacho watu wanaweza kukipata kwa urahisi mtaani kwao —basi hutopata wateja mtandaoni. 

Kwanini wanunue kwako wakati bidhaa hiyo hiyo inapatikana kwa mangi au na maduka mengine ya karibu?

Jiulize; unaweza kuuza soda mtandaoni? Au wembe au majani ya chai? 

Kama kila mtu anauza kile unachotaka kukiuza mtandaoni basi inabidi uwe na OFA nzuri, au kuwe na ubunifu na namna ya uwasilishaji bidhaa yako kwa watu ili kujitofautisha na wengine. Vilevile ujenge mahusiano mazuri na wateja wako ili waendelee kurudi na kuwaambia wengine.

Lakini kwa bidhaa kama vile karanga, mchele, vitenge, na baadhi ya nguo  —hizi zinapatikana kila mahali. Usishangae kuona hupati wateja mtandaoni. 

Watu hawatafuti mtandaoni vitu ambavyo vinapatikana kila kona mtaani kwao. 

Ili kupata wateja mtandaoni, bidhaa yako inatakiwa kuwa na upekee, ubora na soko lake liwe halijachuja (saturated) kwa kuwepo wa utitiri wa bidhaa hiyo kila mahali. Tofauti na hapo, ni bora ufungue duka mahali penye mzunguko mkubwa wa watu (foot traffic). Kama vile Kariakoo.

Mitandao inasaidia kufikisha bidhaa yako kwa watu wengi. Lakini kuuza inategemea na bidhaa yenyewe.

Jina Lako Mtandaoni (Brand Authority)

Kule Instagram wapo watu wanauza bidhaa za aina mbalimbali kama vile nguo, viatu, na electronics. Lakini yapo majina machache maarufu kama vile (kwa Tanzania) Vunja Bei, Frank Knows, David Sportwear, na kadhalika.

Hao na wengine wengi wenye waliojitengenezea jina mtandaoni wanapata wateja na kuuza bidhaa zao.

Unajua kwanini wanauza? Ni kwa sababu watu hupenda kununua kitu kutoka kwa mtu wanayemfahamu, au wamewahi kumsikia, au watu wengine wanamuongelea.

Je wewe umetengeneza jina? Hakuna mtu yuko tayari kukutumia pesa ikiwa hakufahamu, hajawahi kukusikia, wala haoni watu wengine wakikuongelea. Hapa watu kukuongelea maana yake angalau kuwe na comments kwenye post zako mtandaoni.

Naomba nitoe mfano. Kuna watu wanauza bidhaa za makampuni ya network marketing au MLM kama vile BF Suma na Forever Living.

Hawa watu wanashida kubwa. Kwanza kabisa wamepigwa pesa yao ambayo hawataweza kuirejesha kuuza bidhaa hizo. Pili wewe siyo daktari, siyo mtaalamu wa lishe, huna pharmacy, na huna zahanati. Isitoshe huna hata mtu mmoja uliyemponya kwa dawa zako. Dawa yenyewe unasema inatibu “magonjwa mbalimbali”. Kwa kifupi hauna authority ya kumshawishi mtu anunue bidhaa kutoka kwako.

Tatizo siyo bidhaa, tatizo ni nani anauza hiyo bidhaa.

Narudia tena; watu hawanunui bidhaa bali wananunua jina la mtu linalohusiana na bidhaa hiyo. Daktari akikuandikia dawa, unaenda kuinunua na kumeza si kwa sababu unaijua hiyo dawa (inaweza isiwe bora) bali kwa sababu unamwamini daktari.

Nikupe mfano mwingine, hivi majuzi tajiri Elon Musk alitangaza bidhaa mpya ya pefume. Ndani ya masaa machache aliweza kuuza chupa 10,000 kwa bei ya dola za kimarekani 100 kila chupa. Jamaa alitengeneza dola milioni moja ndani ya masaa tu.

Hiyo ndiyo nguvu ya kuwa na jina. Tengeneza jina kwanza halafu kuuza mtandaoni itakuwa rahisi. 

Kutengeneza jina mtandaoni si kuwa maarufu (fame, celebrity). Ni kujenga taswira yenye kuaminika miongoni mwa watu unaowalenga. 

Kumbuka, Kuwa na Jina Mtandaoni Siyo Umaarufu. 

Hapo awali nimesema ili uuze mtandaoni lazima uwe na jina. Hapa simaanishi umaarufu (fame, celebrity). Hapana. Jambo la msingi ni kuhakikisha unatengeneza jina miongoni mwa watu unaowalenga kununua bidhaa yako. Si lazima Watanzania wote wakujue. 

Kama watu 1000 wamekufollow baada ya kuona unachouza basi hilo ndilo jeshi lako. Kama wamekufollow kwa hiari maana yake wamevutiwa na unachokifanya. Endelea kuwapa maudhui bora (waelimishe, wachekeshe, wape mbinu za kutumia bidhaa yako n.k). Hao watu 1000 wanaweza kusambaza habari zako kwa wengine na hivyo ndivyo utakua na kujipatia jina. 

Lengo ni kujiweka katika mazingira mazuri ya kuvutia wateja. Hakikisha profile inavutia, haina makosa au picha zisizo na ubora.

Hapa pia naomba nikazie jambo; kununua followers ni kupoteza pesa zako. Epuka mtu anayekwambia atakupatia followers. 

Uwezo wa Kushawishi Wateja 

Unaweza kuwa na bidhaa nzuri lakini ukashindwa kushawishi wanunuzi. Unaweza kuwa na dawa inayotibu kansa lakini watu wasiamini kwa sababu huna ushawishi. 

Hii ni changamoto ya kushindwa kufahamu saikolojia ya mteja unayemlenga pamoja na kushindwa kuandaa maudhui (content) yenye mvuto na yenye kushawishi. 

Jiulize; zile picha, video na maandishi unayopost mtandaoni yana nguvu ya kushawishi? Yana mvuto? Picha ni kali au ni low quality?

Yote hayo yanachangia kama watu watavutiwa na kukuamini au hawatavutiwa na kukutilia mashaka.

Kwa mfano tuseme unauza pazia. Badala ya kusema; OFA! Jipatie Mapazia Mazuri kwa Bei Nafuu. Tunapatikana Kariakoo

Unaweza kusema; Pendezesha Nyumba Yako kwa Pazia Nzuri Ili Wageni Wakija Waone Kweli Wapo Ndani Ya Nyumba

Wanawake hawanunui pazia bali wananunua UFAHARI wa kupendezesha nyumba. Wakienda kununua pazia swali wanalojiuliza kichwani ni “Pazia gani litapendeza ndani ya nyumba yangu?”. 

Jaribu kucheza na saikolojia ya mteja unapoandaa maudhui ya kupost Instagram au popote unapopatia wateja. Onyesha Matokeo; nini mteja atapata akinunua bidhaa yako? Je atapata mwonekano mzuri? Je chumba chake kitapendeza? 

Katika kuandaa maudhui, onyesha matokeo ya bidhaa. Usionyeshe bidhaa.

Badala ya kupiga picha mabaro ya vitenge dukani kwako, piga picha ya mwanamke aliyevaa kitenge na kupendekeza. 

Badala ya kupiga picha mapazia uliyotundika dukani mwako, piga picha pazia zilizotundikwa ndani ya nyumba. Watu hujaribu kutengeza picha kichwani ya namna gani nguo itaonekana wakiivaa, au pazia litaonekanaje likiwa ndani ya nyumba. Usionyeshe tu bidhaa, onyesha matokeo. 

Ukiwafahamu wateja wako vizuri, na bidhaa yako ikawa iko vizuri, basi hata yale matangazo ya kulipia yatazaa matunda. Vinginevyo utakuwa unachoma pesa.

Hitimisho: Ukweli Kuhusu Kupata Wateja Mtandaoni 

Mitandao ni njia tu ya wewe kufikisha bidhaa yako kwa walengwa. Kuhusu kuuza au kutokuuza inatokana na sababu nyingi ikiwemo bidhaa yenyewe, soko, pamoja na uwezo wako wa kushawishi. 

Kwa ujumla mitandao imerahisisha sana jinsi ya kufikia wanunuzi wa bidhaa za watu. Bila mitandao kama WhatsApp, Instagram, YouTube, Tovuti na mingineyo, watu walio mbali wasingeweza kuona bodhaa yako na kuwasiliana nawewe. 

Kila mtu anaweza kuuza chochote mtandaoni mathalani kitu hicho kina soko na muuzaji anaweza ku-supply hiyo bidhaa.

____________

Asante kwa kusoma makala hii. Naitwa Shukuru Amos, ni mwandishi na mtaalamu wa masoko ya digitali (Digital Marketing). Wasiliana nami kwa WhatsApp hapa

Share makala hii kwa mfanyabiashara mwingine.

Jinsi Ya Kumsaidia Mjasiriamali Mdogo Kukuza Biashara Yake Mtandaoni

Jinsi Ya Kumsaidia Mjasiriamali Mdogo Kukuza Biashara Yake Mtandaoni

Hakuna mtu ambaye anaweza kufanikisha jambo bila msaada wa mtu au watu wengine. Tunaishi kwa kutegemeana. Unachokitafuta wewe kipo kwa mtu mwingine.

Katika dunia yetu ya kidigitali, ni rahisi kuwa sehemu ya msaada mkubwa kwa wajasiriamali wanaotafuta kukuza biashara zao mtandaoni. Unaweza kufanya hivyo bila hata ya kutumia pesa.

Jinsi ya kusaidia kukuza biashara ya mjasiriamali mtandaoni

Follow page yake ya biashara. Inaweza kuwa ni instagram, twitter au facebook – popote unapoona unaweza kumfolllow fanya hivyo. Hii haigarimu pesa yoyote.

Toa Comment , Like au Share post za bidhaa zake ili zipate kuonekana kwa wengi. Kumbuka wewe binafsi una followers ambao nao wana followers, hivyo ukishare au kucomment kweny post ya mjasiriamali huyu, unaipa nafasi post yake kufika mbali zaidi. Hii nayo haikugarimu hela.

Toa maoni, reviews auratings kuhusu huduma yake kwenye page yake Google My Business, kwenye App yake playstore, au kwenye listing directories zingine.

Weka picha ya eneo au bidhaa yake na shiriki kuhakiki (verify) taarifa zake kwenye ramani za google.

Pia wajuze marafiki zako juu ya bidhaa zake.

Cha mwisho, acha kuponda biashara ya mtu mtandaoni. Kama kuna kitu unaona anakosea ni busara kumtumia ujumbe inbox na kumweleza.

Ukifanya yote haya, utakuwa umetumia kiasi cha shilingi SIFURI!

Lakini utakua umemwezesha mtu kufikisha bidhaa yake kwa walengwa hivyo kujipatia kipato cha kuendesha maisha yake. Si lazima uwe na pesa kusaidia, japo ni vizuri zaidi kutoa ukiwa na uwezo huo.

Kama somo limeeleweka, naomba follow page za Tanzlite Digital kwenye mtandao wa LinkedIn, Facebook, Twitter na Instagram. Pia nenda kafanye hivo kwenye biashara ya mjasiriamali unayemjua.

Kugusa maisha ya watu wengine si lazima uwe Bill Gates. Kusaidia kukuza online visibility ya biashara ya mtu ni aina nyingine ya philanthropy!. Tuendelee kuinuana. Usisahau kushare post hii 🙂

Natumaini makala hii imekusaidia. Naitwa Shukuru, ni mwandishi na mtaalamu wa Digital Marketing. Nipate kupitia mtandao wa WhatsApp hapa.

Fahamu Makundi Matatu ya Wateja Mtandaoni (na Jinsi ya Kuwapata)

Fahamu Makundi Matatu ya Wateja Mtandaoni (na Jinsi ya Kuwapata)

Idadi ya Watanzania wanaotumia internet imefikia milioni 27. Katika mamilioni haya ya watu, kuna wateja wengi sana kwa ajili ya biashara yako. Lakini UNAWAPATAJE? Au wanakupataje? 🤔

Kabla hujaanza kutumia njia yoyote ya kidigitali kupata wateja mtandaoni, ni vyema ukafahamu makundi matatu ya wateja wanaopatikana mtandaoni. Itakusaidia kuandaa mpango (digital strategy) utakaoleta matokeo mazuri.

Makundi Matatu ya Wateja Mtandaoni 

1.Wateja wanao kufahamu: hawa ni wale ambao tayari wanajua biashara yako. Wanaweza kuwa ni followers kwenye account zako za mitandao ya kijamii, au una email list yao au wame-subacribe kupata huduma yako. 

Hawa ni rahisi kuwauzia bidhaa yako. Watu wakikufollow ujue tayari wamevutiwa na unachokifanya. 

Kazi yako ni kuwapa huduma bora ili wakakutangaze kwa wenzao. Fanya kila uwezalo kuhakikisha hili kundi haliondoki (Customer Retention

2. Kundi la pili ni wateja wanaohitaji bidhaa yako lakini hawakujui. Hawa wanaweza kuwa wanapata bidhaa hiyo kutoka kwa mtu mwingine au hawajui wapi pa kuipata. 

Kama wanaipata bidhaa hiyo kutoka kwa mtu mwingine maana yake tayari una mshindani. Hapa unakuwa na kazi ya ziada ya kumchunguza mshindani wako. Anatumia mbinu gani kupata wateja na bidhaa yake ni bora kiasi gani kulinganisha na yakwako. 

Je anatumia influencers? Maudhui yake ni bora kiasi gani? Ni mtandao gani wa kijamii amejikita zaidi? Ukifahamu haya na mengine utaweza kuja na mkakati (digital strategy) imara wa kukuza biashara yako. 

Kwa kuwa kundi hili ni la watu wenye UELEWA juu ya wanachohitaji, wengi hutumia search engines kutafuta bidhaa hiyo (they are actively searching online). Hivyo njia nyingine ya kuwapata ni kuwa na mpango imara wa SEO (Search Engine Optimization) au kutumia matangazo ya Google Ads

3.Kundi la tatu ni la wale ambao wangependa kutumia bidhaa yako lakini hawajui kama wanahitaji (they don’t know if they need it). Hapa sasa inabidi uwe vizuri kwenye kitu tunaita Content Marketing. Kundi hili la wateja wanahitaji kuelimishwa sana kabla hawajafanya maamuzi ya kutoa hela yao kununua huduma yako. Wanahitaji elimu juu ya tatizo walilo nalo na kwamba kuna suluhu ya tatizo hilo ambayo ni hiyo bidhaa yako. 

Mara nyingi ukiwa umegundua solution mpya juu ya tatizo fulani, tuseme ni software, tiba lishe au kitu chochote —watumiaji wa solution yako mara nyingi wanakuwa kwenye hili kundi la tatu. Wanahitaji maudhui ya kutosha kuwafundisha tatizo lililopo, madhara ya tatizo hilo na faida za kutumia bidhaa yako. 

Hitimisho

Kumbuka biashara ni watu. Kufahamu makundi ya wateja na tabia zao mtandaoni itakusaidia kuandaa mpango wa digitali wenye kuleta mafanikio katika biashara yako. Hasa upande wa maudhui kwani makundi haya matatu yanahitaji aina tofauti ya maudhui.

Ukiwapa huduma bora wateja waliopo kwenye kundi la kwanza hapo juu, wanaweza kuwa mabalozi wazuri kwa wateja wa kundi la pili na la tatu.

Natumaini makala hii imekusaidia. Naitwa Shukuru, ni mwandishi na mtaalamu wa Digital Marketing. Nipate kupitia mtandao wa WhatsApp hapa. Au jiunge na group letu la Wafanyabiashara wadogo mtandaoni kwa Tsh 7500.

Jinsi ya Kutumia WhatsApp Business Kukuza na Kutangaza Biashara Yako

Jinsi ya Kutumia WhatsApp Business Kukuza na Kutangaza Biashara Yako

Mtandao wa WhatsApp umetutoa mbali sana. Kutoka kwenye status za  kuandika mpaka status za picha na video. Kutoka kwenye magrupu yenye ukomo wa watu 60 mpaka sasa magrupu ya watu nyomi hadi 257. 

Ni wazi kwamba mtandao wa WhatsApp umezidi kuwa bora ili kuendelea kuwafurahisha watumiaji wake. Bora ukose application zingine kwenye simu lakini si WhatsApp.

WhatsApp imekuwa zaidi ya sehemu ya kuchat na kutumiana jumbe zenye kufurahisha (meme), bali ni fursa ya kibiashara kwa wajanja. 

Watu wanataka kuuza, watu wanataka kujiweka karibu na wateja wao. Wengine ndio kwanza wanafungua biashara zao wakitafuta namna ya kujitangaza. WhatsApp imekuwa kimbilio la wajasiriamali wengi wa kitanzania. 

Watu wameanzisha magrupu ya WhatsApp kwa lengo la kuendesha semina na mafunzo mbalimbali. Kuendesha vikundi vya kukopeshana, maarufu kama ‘vikoba’. Vilevile magrup haya yanatumika kuhamasisha watu kujumuika kwenye matamasha na warsha mbalimbali. 

Siku hizi hata vikao vya Sendoff na harusi vinaendeshwa kwenye magrupu ya WhatsApp. Kama bado umejiunga kwenye magrupu ya kipuuzi, basi umebaki wewe tu na wapuuzi wachache. Wenzako tunasaka fursa! 

Yani siku hizi kupata namba ya mtu ni rahisi sana kwa sababu anajua baadaye utaona matangazo ya biashara yake kwenye status. Wala si kwa ubaya, ni katika harakati za kutafuta masoko na kujipatia riziki. Wewe ambaye huna cha kutangaza usione kero.

Hatufahamu ni mazuri yapi mengine wamiliki wa mtandao wa WhatsApp wametuandalia, lakini kizuri kimojawapo ni kuhusu application ya WhatsApp Business.

WhatsApp Business ni nini na ina tofauti gani na WhatsApp ya Kawaida?

Two whatsapp icons

Kwanza kabisa, WhatsApp Business ni application halali inayomilikiwa na kampuni ya WhatsApp Inc. Hii sio kama zile WhatsApp GB na zinginezo (not a third-part App) ambazo huwa zinakataliwa. Hii ni maalumu kwa wafanya biashara na wajasiliamali wanaotaka kupromote biashara zao pamoja na kuimarisha mahusiano na wateja wao. Lakini hata wewe usiye na biashara unaweza kuitumia kwa mawasiliano ya kawaida.

Makampuni kama Bloomberg na Mwananchi wanatumia WhatsApp Business API (huduma advanced hii ni huduma ya kulipia) kutuma updates kwa subscribers wao moja moja kwenye inbox zao.

Mtandao wa WhatsApp umekuwa kimbilio kwa wajasiriamali wengi nchini Tanzania.

Sasa tuiangalie WhatsApp Business kiundani zaidi. Vitu ambavyo utavipata ndani yake ni kama  ifuatavyo;.

  • Business profile 
  • Ujumbe automatic wa salamu
  • Customer Management
  • Takwimu/statistics
  • Majibu ya haraka (quick replies)

Business Profile

Ukiangalia profile ya mtu anayetumia WhatsApp Business utaona ina muonekano tofauti na ile ya kawaida.  Hapa utaona vitu kama jina la biashara, maelezo ya biashara (business description), location pamoja na siku na masaa anayofungua biashara yake. Hivi ni vitu ambavyo huwezi kuviona kwa mtu anayetumia WhatsApp ya kawaida.

Customer Management

Hapa unaweza kuchambua na kupangilia namba za WhatsApp ulizonazo katika makundi mbalimbali ya wateja. Kwa mfano unaweza kumwekea alama (label) kama vile mteja mpya, aliyelipa, asiyelipa, aliyetoa oda mpya na aliyemaliza oda yake.

Ujumbe Automatki wa Salamu

Hapa unaweza kutengeneza ujumbe wa salamu utakao kuwa ukitumwa kwa kila anayekutumia meseji. Ili kuondoa kero na usumbufu, ujumbe huu hutumwa endapo tu hamjawasiliana kwa kipindi cha siku 14. Ujumbe huu wa salamu unaweza kuwa unaelezea kwa ufupi juu ya shughuli unayofanya. Ni namna ambavyo wewe utapenda iwe. 

Takwimu

Katika application ya WhatsApp Business, unaweza kupata takwimu kuhusu meseji ulizotuma. Utaweza kuona idadi ya meseji ulizotuma, zilizofika na zilizosomwa.

Quick replies and away message

Sikushauri utumie sana hii feature kwani humfanya mtu ajisikie kama ana wasiliana na roboti badala ya mtu. Kama namba yako ya mawasiliano ya kawaida ndiyo hiyo hiyo unatumia kwa biashara zako bora usitumie hii setting kwani si kila mtu ni mteja wako.

Jinsi ya kuwezesha WhatsApp Business

Ni rahisi sana kuseti business profile kwenye application ya WhatsApp Business. Unachotakiwa kufanya ni kwenda Playstore ama Appstore na kudownload WhatsApp Business. Baada ya hapo fungua application na uende kwenye Settings.

Kama unatumia android bofya kwenya vidoti vitatu upande wa juu kulia > Settings > Business settings >  Hapo utaona setting zote unazotaka kufanya.

Mwisho…

Dunia ya sasa ni dunia ya kujiuza (simaanishi kujiuza unakofikiria wewe). It is all about branding yourself. Kama hutokuwa na ujasiri wa kusimama na kuonyesha ujuzi na maarifa yako, unataka nani akufanyie hivyo?

WhatsApp ni moja kati ya jukwaa zuri kuji-brand. Mara moja moja si mbaya kupost utani (meme) lakini isiwe kila siku wewe ni wa kupost upuuzi tu. Usifikiri ni utani tu, people are more likely to associate you with the things you post online. Jenga taswira chanya ili uweze kuvuta fursa zije upande wako.

Unatuamiaje WhatsApp yako? Tuambie uzoefu wako.

TANGAZO: Tumeanzisha group la WhatsApp kusaidia wajasiriamali wanaouza bidhaa mtandaoni. Bofya picha hapo chini.