Mbinu Mpya Ya Kupata Kazi Ukihitimu Chuo

Mbinu Mpya Ya Kupata Kazi Ukihitimu Chuo

Soko la ajira ni changamoto kubwa inayosumbua vichwa vya wanafunzi wengi hasa wale wanaohitimu vyuo vikuu katika nyakati hizi. Jambo ambalo linafanya vijana wengi wakose imani ya kufanikiwa tena.

Kwanza ijulikane kuwa degree peke yake sio kigezo cha mhitimu kupata kazi kwa sababu wengi huamini akimaliza chuo kazi ni yake. Sasa hivi bila kujiandaa mapema mambo ni magumu sana, soko la ajira ni gumu.

Hata hivyo, kupenya kwenye soko la ajira ni jambo linalohitaji juhudi, ujuzi na utayari wa mtu mwenyewe. Katika makala hii, tutaangazia jinsi mwanachuo anavyoweza kupenyeza kwenye soko la ajira.

Je, ni nini unachoweza kufanya kama mwanachuo ili kuongeza uwezekano wa kupata kazi?

Mchakato wa kutafuta kazi unapaswa uanze mapema, hata kabla ya kuhitimu. Je wewe ni mwanachuo?

Kama jibu ni Ndiyo, basi unaweza kuanza kutafuta fursa za kazi mapema mtandaoni au kwa kushiriki katika programu, miradi, semina, kuandaa projects na kujitolea katika makampuni.

Kwa kushiriki na watu wengine utapata kuongeza marafiki wapya (connection) ambao baadae wanaweza kuwa ndio daraja lako la kupata kazi.

Pia ukianza kujitolea mapema ukiwa chuo utapata uzoefu wa kazi mapema through internship/freelancing ambao utakusaidia kuwa na ujuzi unaohitajika kwenye soko la ajira pindi tu umalizapo chuo.

Ivi ulishawahi kusikia au kuulizwa hili swali, unauzoefu wa miaka mingapi? chukulia ndio tu umemaliza chuo halafu unaingia interview kuulizwa hilo swali, utajibu nini? Hivyo anza mapema kutafuta makampuni ujitolee au ufanye freelancing ili baadae swali hili lisikusumbue.

Ni nini kinachotarajiwa kutoka kwako katika soko la ajira?

Unaweza kujenga mtandao wako wa kijamii (networking) kwa kuwa na mahusiano mazuri na walimu, wanafunzi wenzako na wataalamu wa tasnia yako. Kupitia mtandao huu, utaweza kupata taarifa za kazi pale zinapopatikana.

Hapa nina maanisha uwe na watu ambao watakuwa wana-support kile unachokifanya. Ukiishi na watu ambao hawasupport unachokifanya maana yake hakuna kazi utapata kupitia wao.

Muhimu: Kwa dunia tuliyopo, kama mwanachuo ataamua kuitumia vizuri mitandao ya kijamii yaani social media platforms kama Linkedin katika kujiuza (personal branding) basi mtu huyu;

Hatakuwa anatafuta kazi bali kazi zitakuwa zinamtafuta yeye by Shukuru Amos.

Soko linahitaji vijana wenye maarifa ya kufanya kazi fulani, kuna kazi zingine hata hazihitaji cheti kikubwa uwe na uwezo wa kutatua changamoto za kampuni husika au uwezo wa kuisadia kampuni ikaongeza mauzo au kupandisha hadhi yake?

Jinsi gani unaweza kuboresha ujuzi wako, kupata maarifa yanayohitajika katika tasnia uliyopo?

Technolojia inabadilika kwa kasi sana hivyo unaweza kutumia mitandao ya kijamii kufuatilia mabadiliko yanayotokea katika tasnia yako na kujifunza ujuzi mpya kupitia kozi mbalimbali mtandaoni ikiwemo Marketing.

Chuoni utapewa Mwongozo tu hivyo kuna kila sababu za kutafuta maarifa zaidi. “Kama elimu ya chuo itashindwa kukufanya kuwa unachotaka basi Professor Youtube na msaidizi wake Google wanaweza”.

Utajiuliza ni kivipi Youtube au google inaweza kukusaidia kutimiza ndoto zako? Unahitaji tu kujua unataka usome nini then weka bundle YouTube anakufungulia dunia kuwa unachotaka.

Je ni sahihi kuweka wasifu wako mtandaoni?

Kutengeneza wasifu wako mtandaoni kunaweza kukusaidia sana katika harakati za kutafuta kazi. Wasifu huo utakuwa hewani 24/7 unasomwa na watu wa aina tofauti tofauti ikiwemo waajiri wako baadae, wateja wako.

Hivyo ni vyema kuweka mawasiliano yako, barua pepe na nambari ya simu katika kurasa zako ili watu wakikuhitaji iwe rahisi kukupata.

Wasifu wako mtandaoni unaweza kuwa fursa nzuri kwa wateja au waajiri wanaotafuta talents mtandaoni kujua zaidi kuhusu wewe, uwezo wako na kitu unachoweza kuwasaidia.

Iwe ni Twiter, Facebook, au LinkedIn we jiweke as a professional wa kitu fulani huwezi kujua huko mbeleni ni fursa gani unaweza kuipata. Who knows what will happen tomorrow?

Nifanye nini ili nitambulike na niweze kupata kazi?

Kujitangaza ni muhimu sana katika ulimwengu wa kidigitali hasa unapokuwa kwenye harakati za kutafuta kazi.

Wewe Mwanachuo unapaswa kuwa na ujuzi wa kujielezea mwenyewe katika majukwaa ya aina yoyote iwe kwa maandishi au kwa kuongea.

Kujifunza jinsi ya kuwa mbele kiujuzi na kimaarifa kunaweza kukusaidia kuwa na ujasiri, uwezo wa kuwasilisha mawazo, kushawishi waajiri wakupe kazi.

Asilimia 90 ya mazungumzo mtandaoni huwa ni kwenye maandishi hivyo ni bora kuwa vizuri zaidi kwenye uandishi.

Bonus: Mtu awaye yote, mwenye kutafuta afueni ya maisha yake, yambidi afanye bidii na juhudi zote katika kutatua matatizo yanayoisibu tasnia yake.