Fahamu Namna Nzuri Ya Kutumia Mitandao Ya Kijamii

Fahamu Namna Nzuri Ya Kutumia Mitandao Ya Kijamii

Je, mitandao inakutumia zaidi kuliko unavyotakiwa kuitumia?. Leo hii mtu akinunua simu kubwa (smartphone) kitu cha kwanza anachokimbilia ni kujipost mtandaoni hata kama yuko kitandani, saa ngapi hajajipost mtandaoni ili wamuone!. Je hivi ndivyo tunavyotakiwa tuitumie mitandao?

Kuwa kwenye ulimwengu wa kidigitali kunafanya watu wengi washindwe kuzikabili hisia zao, jambo lolote linalofaa machoni pake anaona ni vyema kulipost mtandaoni. Wengi hatuna uelewa hasa vijana kuhusu namna nzuri ya kuitumia mitandao ya kijamii katika miradi ya kutusaidia baadae.

Sasa wewe unajipost kila siku mtandaoni aisee, angali sana ujue u bado kijana ambaye hujui hata kesho yako itakuwaje. Picha yoyote unayopost mtandaoni hiyo imeenda, watu wataiona  na itahifadhiwa kwenye algorithms milele na milele hata wajukuu zako ipo siku wataiona.

Hivyo jitahidi sana unapo-post kitu chochote kwenye social media angalau kiwe chenye maadili na inatunza heshima yako na inaleta mantiki kwa mtu yeyote. Kuna siku watu watakujaji kupitia picha hizo ulizopost huko Instagram au Twitter.

Ubaya zaidi saivi mambo yapo kidigitali zaidi kwamba mtu akitaka kukujua zaidi anakusearch mtandaoni akikutana na mambo yako ambayo siyo mazuri basi utapishana na gari la mshahara.

Kuliko kupost picha ya mpenzi wako, familia au kuonyesha maisha yako kwa njia ya picha ni bora ukatumia muda huo angalau kujifunze digital skills zitakazokusaidia kutengeneza ajira yako mwenyewe.

Chukulia mfano huu, kampuni fulani inataka ikuajiri je, ikiangalia picha zako mtandaoni utafaa kweli kupewa hiyo kazi? au watakuona kama mhuni fulani? Hii ni kwa sababu jinsi unavyojipost ndivyo unavyojielezea zaidi kuwa wewe ni nani, ni wa aina gani, unafanya nini, unapenda nini, uko makini kiasi gani?

Picha zako mtandaoni ni ushahidi tosha watu kukujua vizuri kuliko unavyojijua.

Mitandao ni sehemu ambayo unaweza kutafuta fursa za kazi, kujifunza maarifa mbali mbali kutoka kwa watu wengine. Lakini kaa ukijua mtandaoni kuna kila aina ya watu kuna watu kazi yao ni kutoa taarifa za upotoshaji, uchi na nyingine amabazo si rasmi hivyo huko mtandaoni chagua watu wa kuwafollow ili usichanganye mafaili ukaingia kwenye mtego wa panya.

Ukiona unapata taarifa ambazo siyo nzuri kwenye feed yako, fanya kuwa unfollow, kuwa block watu wote ambao maudhui yao hupendezwi nayo. Ikiwezekana zima notification za mitandao ya kijamii unayotumia kwenye simu yako ili isikuletee shida, kila dakika notification zinatokeza pale juu kwa hali hii si utakosa f ocus sasa!.

Itumie mitandao katika miradi hiyo na si kuvimbiana au kujionyesha kana kwamba upo kwenye maonyesho.

Ziko wapi ajira? Ni sauti ya kila kijana baada ya kuhitimu chuo. Mitandao ni fursa shituka, tangaza kitu kinacholeta mantiki kwa watu usitangaze hisia zako.

Saa nyingine huwa nasema hata WhatsApp kwa mwanafunzi ni sehemu nzuri ya kujitangaza kuhusu ujuzi wake you never know mtu anayeangalia status yako huenda siku moja atakuwa anafanya kazi sehemu na akakuita kufanya kazi na wewe sababu tu anajua una ufahamu wa mambo fulani. Usipost tu memes fikiria hilo pia.

Kwenye game ya kutafuta kazi mtandaoni huwa iko katika swali hili “unaweka nini kwenye akili za watu pale wanapoona ulichokipost?” Yaani mtu atafikiria nini kuhusu wewe kulingana na ulichokipost. Ifikie mahari uwe na fikra za mbali baada ya miaka mitano mbele, kile ulichokipost kitakutambulisha kama nani? 

Tunaishi kwenye ulimwengu wa kidigitali ambao mtu anaweza kufanya kazi remotely, itafika muda baadhi ya ajira kama siyo zote zitakuwa zinatolewa baada ya waajiri kukuona mtandaoni unafanya kitu fulani ambacho wanauhitaji nacho.

Kutafuta kazi ni kazi. Saivi soko linakoelekea ni kwamba watu wengi watakuwa wanafanya kazi remotely, kama ambavyo freelancer wanavyotafuta kazi akishaipata na kuifanya ndo imeisha.

Na atakayepata bahati hii ni yule ambae account zake za mitandao ya kijamii inajieleza yenyewe vizuri kuhusu yeye, na yuko active. Hakutakuwa na kutuma maombi wala interview labda iwe ni lazima. Mtu huyu atashuhudia message ikiingia au akipigiwa simu zikisema



Habari,

Nimekuona kwenye mitandaoni ukielezea zaidi kuhusu blablaa ah! nimekuwa nikikufuatilia toka muda …, vipi unaweza kunisaidia kufanya hili jambo fulani?

Noah Harari Mwanahistoria alisema “We are going to believe more on algorithms than we believe in ourselves”.

Wengi bado hawaamini katika hili lakini ndo tunakoelekea miaka mitano ijayo digital platforms zitakuwa ndio kimbilio kwa makampuni, agencies na watu binafsi.

Wewe bado kijana jitahidi profile za akaunti zako ziko safi huku mtandaoni halafu kujipost siyo issue achana nayo.

Kuna kitu kinaitwa Social media profiling hutumiwa sana na wadukuzi wa taarifa mtandaoni, watu wa IT na cybersecurity wanaelewa vizuri, hii inaweza kutumika kupata taarifa zako nyeti, Vitu unavyopost Instagram, Twitter, Tiktok, vinaweza kumpa mdukuzi taarifa nyingi kuliko unavyofikiria japo wewe huwezi elewa.

Na kibaya zaidi saivi watu hawaamini udukuzi, hawaamini kabisa haya mambo ya kuhakiwa utasikia “hii technolojia bado sana kwetu, nani atani-hack mimi wakati hata pesa sina?” siku yakikutokea mimi sitakuwepo lakini nimekwambia haya mambo yapo.

Tabia ya kupost maisha yako au familia yako kwenye mitandao siyo nzuri na inaweza kukugharimu baadae.

Halafu kuna watu wanasoma cybersecurity nchi hii, subiri baada ya miaka mitano tutakuwa na vijana wengi ambao hawana ajira na kazi yao itakuwa ndiyo hiyo KUHACK maybe sharia (Cybercrime Act 2015) iwekewe mkazo.

Tumia mitandao ya kijamii katika namna ambayo haitakuja kuharibu heshima yako bali itakutangaza vyema kwenye digital world.

Je mtandao wa kijamii wa TikTok waweza kuwa fursa kwa biashara?

Je mtandao wa kijamii wa TikTok waweza kuwa fursa kwa biashara?

Maisha yanakimbia kwa kasi sana. Miji inazidi kuwa ya kisasa na yenye kupendeza. Umri nao unatutupa mkono vilevile. 

Siku hizi ukilala, ukiamka kuna jambo jipya limeibuka. Mitindo tofauti tofauti ya mavazi, muziki na mengine inakuja na kuondoka kama maji yatiririkayo chini ya daraja la mto uendao kasi. 

Ukija upande wa teknolojia ndio usiseme kabisa. Leo iPhone imetoka mpya kesho Samsung katoa kitu kikali zaidi. Hujakaa sawa Huawei anamtikisa Mmarekani kwa teknolojia ya 5G. Hapa tunaoteseka ni sisi. Hela zenyewe ziko wapi za kuweza kuwa na kila toleo jipya? Wacha tubaki na tecno zetu bwana! 

Turudi kwenye mada yetu;

Tunapozungumzia biashara za karne ya 21, tunagusa moja kwa moja maswala ya digitali, likiwemo suala la mitandao ya kijamii. Mitandao hii imekuwa nguzo muhimu kwa wafanyabiashara kuweza kutangaza bidhaa na huduma zao pamoja na kujenga mahusiano mazuri na wateja wao. 

Ninafahamu unatumia mitandao ya kijamii hasa ile maarufu kama Instagram, Facebook na Twitter. Huenda ukawa umekutana na makala hii kwenye moja ya mitandao hiyo. 

Lakini kuna mtandao mmoja unakuja kwa kasi sana kwa sasa. Unaitwa TikTok. Endelea kusoma kuona ni nini kipya juu ya mtandao huu. 

Takwimu zinasemaje kuhusu mtandao wa TikTok?

Kwa kipindi cha miaka minne tangu kuanzishwa kwake mwaka 2016, TikTok imeweza kuwa na watumiaji zaidi ya milioni 500 duniani kote. Wengi wa watumiaji hawa wakiwa ni vijana. 

Ripoti ya Globalwebindex ya mwaka 2019, inaonyesha asilimia 41 ya watumiaji wa TikTok wana umri kati ya miaka 16 na 24 (Globalwebindex, 2019). Kati ya watumiaji hao, watu zaidi ya milioni 150 hutumia application hiyo kwa siku. 

Aidha, imeripotiwa kuwa application ya TikTok imeongoza kwa kupakuliwa (downloaded) kwenye App Store ya Apple mwaka huu wa 2019. Kuhusu takwimu zaidi, tembelea chapisho la Kiingereza kupitia kiungo hiki

TikTok ina kipi cha tofauti?

TikTok inawapa watumiaji uhuru wa kutengeneza vipande vifupi vya video (visivyozidi sekunde 15) vikinakshiwa na nyimbo na urembo mwingine (filters) wa kuvutia kwa kutumia simu zao za mkononi. Video hizi zimejaa furaha na ucheshi (funny). 

Ukitofautisha na mitandao mingine kama Twitter na Instagram, mitambo (algorithm) ya TikTok inakuonesha vitu unavyovitaka tu. Sio mara unakutana na post ambayo hata hujui imetoka wapi kama inavyotokea huko Twitter na Insta. Pia matumizi ya hashtag yanatamba sana kwenye mitandao huu. 

Wanasema utamu wa ngoma ingia mwenyewe ucheze. Pakua application ya TikTok uonje utamu wake.

Ukiitizama vizuri application ya TikTok utaona ina muonekano sawasawa na application inayoitwa Musical.ly. Hii ni kwa sababu TikTok ambayo ni kampuni ya Kichina, iliinunua application ya Musical.ly ili kuweza kuwafikia watu wengi hasa vijana wa kimarekani. 

Swali; Je TikTok inaweza kuwa fursa mpya kwa wafanyabiashara? 

Kwasasa TikTok haina mfumo wowote unaowezesha kuweka matangazo ya kulipia (sponsored ads) kama tunayoyaona huko kwenye mitandao mingine. 

Lakini kama tunavyofahamu, hakuna kitu cha bure. Nionavyo mimi, jukwaa hili halitakuwa la bure kwa mda mrefu.

Kwa kuwa mtandao huu unapendwa na vijana wengi ambao ndio wenye nguvu ya ushawishi katika masoko, ninaona kuna kila dalili ya makampuni makubwa (brands) kuishawishi ikubali TikTok ikubali matangazo. 

Baadhi ya takwimu zinatabiri mtandao wa TikTok utakuja kuteka na kuizidi mitandao kama vile Instagram na Snapchat.

Changamoto kubwa ya mitandao ya kijamii ni tabia yake ya kubadilika kila mara, kwa kuja na mifumo mipya au kupotea kabisa kama mtandao uliokuwa ukimilikiwa na kampuni ya Google, uliofahamika kwa jina la Google+

Lakini pia ni lazima tukubaliane na ukweli kwamba hatuwezi kukwepa social media. Mitandao hii imewapa nguvu watumiaji kuwa na uhuru wa kuchagua ni namna gani wanataka kupokea taarifa. Hivyo kama mfanyabiashara unaetafuta kukuza jina la biashara yako na kufikia wateja wengi zaidi, huna budi kuwekeza kwenye moja ya mitandao hii. 

Palipo na wengi pana fursa nyingi. Wewe kama mfanyabiashara, unajiona uko tayari kuwafata wateja wako walioko TikTok? Au utawasubiri wakirudi Insta na Fb?